Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Mradi wa stadi za maisha wasaidia kurejesha wasichana walioacha shule Tanzania

Mkurugenzi wa Camfed Nasikiwa Duke akiwasilisha taarifa ya namna program ya Stadi za Maisha ilivyo pokelewa mbele ya kikosi kazi cha Taifa.
John Kabambala
Mkurugenzi wa Camfed Nasikiwa Duke akiwasilisha taarifa ya namna program ya Stadi za Maisha ilivyo pokelewa mbele ya kikosi kazi cha Taifa.

Mradi wa stadi za maisha wasaidia kurejesha wasichana walioacha shule Tanzania

Utamaduni na Elimu

Mwaka 2013, Tanzania ilishuhudia mwanzo wa mabadiliko makubwa katika elimu ya msingi na sekondari kupitia mradi wa kusisimua ulioanzishwa na Shirika la Campaign for Female Education – CAMFED. Mradi huu ulikuwa na lengo la kuboresha stadi za maisha kwa wanafunzi wa kike na kuwapa fursa zaidi za elimu na ujifunzaji.

Mradi huu unaotekeleza lengo namba 4 na namba 5 ya malengo ya maendeleo endelevu SDGs ya Umoja wa Mataifa yanayohimiza Elimu bora na Usawa wa kijinsia mtawalia umeleta mabadiliko chanya katika elimu na maisha ya wanafunzi wa kike nchini Tanzania.

Kwa mujibu wa malengo ya program hii, shirika kwa kushirikiana na Serikali linatarajia kufikia asilimia 85 ya Shule zote nchini Tanzania ifikapo mwaka 2030, ikiwa ni moja ya njia ya kuunga mkono Malengo 17 ya Maendeleo Endelevu ya kudumu ya Umoja wa Mataifa SDGs.

Soundcloud

Ushirikiano na serikali 

Kama ilivyo kwa maeneo mengi duniania, wanafunzi wa kike nchini Tanzania wamekutana na changamoto nyingi katika kupata elimu bora na kufikia malengo yao ya elimu. Hali hii ilitokana na sababu mbalimbali zikiwemo umaskini, mila na desturi potofu, na upungufu wa rasilimali za elimu. Shirika la CAMFED linalofanya kazi katika nchi kadhaa za Afrika, lilichukua hatua kwa kushirikiana na serikali ya Tanzania kupitia wizara ya Elimu sayansi na utamaduni pamoja na Ofisi ya Rais, Tawala za mikoa na Serikali za Mitaa TAMISEMI na wadau wengine kuanzisha mradi wa Stadi za Maisha kwa Wanafunzi wa Kike kwenye shule za Sekondari.

Kwa mujibu wa Mkurugenzi wa washirika hilo la Camfed nchini Tanzania Bi, Nasikiwa Duke wakati mradi huo wa Stadi za Maisha unaanza walizifikia Shule 365 za Sekondari lakini hadi kufikia mwaka huu wamezifikia Shule 466, ambazo zina nufaika na program ya Stadi za Maisha.

CAMFED  iliwezesha elimu ya mafunzo ya stadi za maisha kwa wanafunzi wa kike ili kuwajengea ujuzi wa kujitegemea, kujitambua, na kushiriki kikamilifu katika jamii. Hii ililenga kuwawezesha kuwa viongozi na wabunifu katika maisha yao. Na ilifanya kwenye jamii ili kubadilisha mtazamo wa jamii kuhusu elimu ya kwa watoto wa kike na kuondoa mila na desturi potofu zinazoweza kuzuia upatikanaji wa elimu kwa wasichanaAmesema bi, Duke.

Programu hii ilichochea maeneo kadhaa ikiwemo kukuza Uongozi na Ujifunzaji, na ilisisitiza uendelezaji wa uongozi na ujifunzaji wa wanafunzi wa kike kupitia kwa walimu walezi na vikundi vya wanafunzi Shuleni. Hii ilisaidia kujenga ujasiri na uwezo wa kushiriki katika masuala ya elimu na kijamii kabla na baada ya kuhitimu masomo yao ya elimu ya Sekondari.

Akiwasilisha upande wa serikali katika utekelezaji wa mradi huu Mussa Mnyeti kutoka Wizara ya Elimu Sayansi na Teknolojia, anaeleza namna programu hii ilivyo na umuhimu kwa Serikali

Programu hii ya Stadi za Maisha ni mkakati unaoisaidia Serikali kupambana na mdondoko kwa wanafunzi hasa wakike, kwani kumekuwepo na changamoto nyingi zinazo wakumba watoto wakike ikiwa ni pamoja na kukatisha masomo kwa sababu ya mimba za utotoni na changamo za kimazingira.” Amesema Mnyeti. 

Mwakilishi huyo wa wizara ameongeza kuwa “Hivyo kupitia mpango huu ambao unahusu kuwafundisha vijana Stadi za Maisha wakiwa bado shuleni, ninaamini kabisa Serikali inauunga mkono, na kumuandalia mazingira mazuri kwa watendaji kazi ilikwamba mdau huyu wa elimu ambae ni Camfed aweze kufikia shabaha ilio kusudiwa”.

Wanafunzi waliokatiza masomo warejea shuleni

Kupitia jitihada hizi, za Stadi za Maisha ziliwezesha mabadiliko makubwa katika maisha ya wanafunzi wa kike nchini Tanzania. Wanafunzi wengi wa kike walipata fursa ya elimu bora na kujifunza stadi muhimu za maisha ambazo zilikuwa muhimu katika kujenga mustakabali wao. 

Pia, program hii iliongeza uwepo wa wanawake katika nyanja za uongozi na uvumbuzi.

Matokeo chanya yaliyo tajwa na mkurugenzi wa shirika la Camfed Tanzania yanathibitishwa na Mkuu wa divisheni ya Elimu Sekondari kutoka halmashauri ya Chalinze Mkoa wa Pwani Bi, Salama Ndyetabura anayeeleza kupitia ofisi yake wamefanikiwa kurejesha wanafunzi walio kuwa wamekatiza masomo kwa sababu mbalimbali, kamavile mimba za utotoni, mazingira magumu na kwa sababu ya mifarakano ya wazazi.

Programu hiyo pia imefanikisha wanafunzi wengi kujitambua na kuchochea ufaulu mkubwa kwa wanafunzi, hasa katika idara ya elimu Sekondari katika halmashauri ya Chalinze. 

Imeandikwa na John Kabambala wa redio washirika Kids Times Fm