Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Guterres: Ushirikiano wa Kusini- Kusini unahitaji zaidi sasa kuliko awali

Shule nchini Guinea- Bissau, mwanachama wa ushirikiano wa kusini -kusini
UNOSSC
Shule nchini Guinea- Bissau, mwanachama wa ushirikiano wa kusini -kusini

Guterres: Ushirikiano wa Kusini- Kusini unahitaji zaidi sasa kuliko awali

Masuala ya UM

Ofisi ya Umoja wa Mataifa ya ushirikiano wa kusini – kusini UNOSSC imefanya mkutano wake wa ngazi za juu kwa njia ya mtandao siku ya ijumaa (10 septemba 2021) ukilenga kukuza mshikamano "kuunga mkono mustakabali wa ujumuishi, wenye ujasiri na endelevu". 

Mkutano huo umefanyika ikiwa ni siku mbili kabla ya Siku ya Umoja wa Mataifa ya Ushirikiano wa Kusini-Kusini, iliyofanyika tarehe 12 Septemba.

Akizungumza katika mkutano huo Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterres amesema "Wakati dunia ikiendelea kukabiliana na janga la COVID-19 na tishio la mabadiliko ya hali ya hewa, ushirikiano wa Kusini-Kusini na wa pembetatu ni muhimu zaidi kuliko hapo awali."

Guterres amesema janga la COVID-19 ni "changamoto ngumu zaidi inayokabili ulimwengu na inadhoofisha mafanikio makubwa ya kijamii, kiuchumi na mazingira. Katika wakati huu wa majaribu ushirikiano wa kusini – kusini, kwa mara nyingine tena umethibitisha kuwa ni muhimu kwa nchi zinazoendelea”.

Ameongeza kuwa katika kipindi chote cha janga hilo la ulimwengu, nchi za kusini zimekuwa zikishirikishana ujuzi na rasilimali katika kusaidiana kwenye juhudi za kukabiliana nalo na kupona. Lakini lazima mengine meng yaendelee kufanyika. 

Katibu Mkuu hiyo wa Umoja wa Mataifa anaamini “Ulimwengu unahitaji ushirikiano wa kina zaidi wa kimataifa kushughulikia mgogoro wa kiafya duniani, kupunguza umasikini, na ukosefu wa usawa, ili kuweza kufikia Malengo ya Maendeleo Endelevu SDGs na kuepusha majanga la hali ya hewa.”

Akizungumza katika mkutano huo, Rais wa Mkutano Mkuu wa Umoja wa Mataifa, Volkan Bozkir, amesema ulimwengu unahitaji kufanya juhudi zaidi kusaidia nchi zinazoendelea ili ziweke kupata unafuu kutoka kwa janga la COVID-19.

"Nina orodha ndefu ya taarifa za ukweli na takwimu zinazoonesha athari kwa nchi zinazoendelea, kwenye maeneo yote, kutoka kwenye masuala ya mapato hadi usawa, kutoka uwezeshaji wa kijinsia hadi kupata huduma za kijamii. Inatosha kusema, takwimu hizi sio nzuri. Miaka ya mafanikio ya maendeleo yamefutwa au yapo hatarini, “

Bozkir ameongeza kuwa, katika safari zake, haswa Asia ya Kati na katika Caribiani, ameona kuwa ushirikiano wa Kusini-Kusini na pembetatu ni muhimu sana katika kushughulikia changamoto, haswa zile zinazovuka mipaka na ukanda. 
Kwake yeye, timu za Umoja wa Mataifa za nchi na kanda zimewekwa vizuri kukuza na kuunga mkono juhudi hizo za kukuza ushirikiano.