Tumemuomba Guterres asiwasahau watanzania katika nafasi za juu za uongozi: Mulamula 

1 Septemba 2021

Waziri wa Mambo ya nje na ushirikiano wa kimataifa wa Tanzania, Balozi Liberata Mulamula amefanya ziara maalum katika makao makuu ya Umoja wa Mataifa mjini New York Marekani, kuwasilisha ujumbe wa rais wa nchi hiyo Samia Suluhu Hassan.

Akihojiwa na Leah Mushi wa Idhaa ya Kiswahili ya Umoja wa Mataifa katika makao makuu yake jijini New York, Marekani Balozi Mulamula  amesema “Katika Mazungumzo yetu na Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterres moja nimemfikishia salamu za pongezi kutoka kwa Rais Samia Suluhu Hassan kwa kuchaguliwa kushika awamu ya pili ya uongozi wake” 

Mulamula pia ameeleza Katibu Mkuu Guterres amepongeza uongozi wa Tanzania katika kipindi kifupi alichokuwa madarakani Rais Samia Suluhu Hassan kwa kuimarisha na kujenga uhusiano baina ya Tanzania na Umoja wa Mataifa. 

Waziri Mulamula ameongeza kuwa amewasilisha ombi maalum wakati huu Guterres akiunda safu ya uongozi wake katika kipindi cha awamu ya pili asiache kuchagua watanzania kushika nafasi  “Wakati wa maongezi yetu na Katibu Mkuu Guterres nimemkumbusha kuwa ni aibu kuona Tanzania ambayo imekuwa ni mshiriki mkubwa katika shughuli za Umoja wa Mataifa lakini tunawafanya kazi kama watatu au wanne ambao wapo kwenye uongozi.”

Mulamula amesema pamoja na kutoa ombi hilo lakini amewakumbusha watanzania kutobweteka na kuchangamkia fursa mbalimbali na wajiongeze kuomba fursa hizo mbalimbali kwa kuwa wanaweza na kwa kuwa balozi wa kudumu wa Tanzania katika Umoja wa Mataifa anafanya kazi nzuri sana yakuwapigia chepuo. 

 

♦ Kurambaza ukurasa mahsusi wa Siku ya Kiswahili Duniani bofya  hapa.
♦ Iwapo ungependa kupokea taarifa kutoka UN News Kiswahili kila wakati zinapochapishwa jisajili  hapa.
♦ Pia unaweza kupakua apu ili kusikiliza matangazo yetu wakati wowote popote ulipo.
♦ Tembelea pia chaneli yetu ya Youtube na pia Soundcloud na Twitter