Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Balozi Mahiga alikuwa mwanadiplomasia aliyejizatiti - UN

Mwakilishi Maalum wa Katibu Mkuu wa UN nchini Somalia, Balozi Augustine Mahiga (kushoto) akiwa na Msaidizi wa Katibu Mkuu kuhusu masuala ya mashinani Ameerah Haq (katikati) mjini Mogadishu, Somalia (13 Novemba 2012)
AU-UN PHOTO / STUART PRICE.
Mwakilishi Maalum wa Katibu Mkuu wa UN nchini Somalia, Balozi Augustine Mahiga (kushoto) akiwa na Msaidizi wa Katibu Mkuu kuhusu masuala ya mashinani Ameerah Haq (katikati) mjini Mogadishu, Somalia (13 Novemba 2012)

Balozi Mahiga alikuwa mwanadiplomasia aliyejizatiti - UN

Masuala ya UM

Umoja wa Mataifa umeelezea masikitiko yake kufuatia kifo cha Waziri wa Katiba na Mambo ya Sheria wa Tanzania, Dkt. Augustine Mahiga kilichotokea leo Alfajiri kwenye mji mkuu wa nchi hiyo, Dodoma.
 

Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa, Antonio Guterres amenukuliwa na msemaji wake akieleza kuwa, “tunahuzunishwa na kifo cha Balozi Mahiga na tunatuma salamu zetu za rambirambi kwa serikali na wananchi wa Tanzania na familia ya marehemu.”

Msemaji huyo Stephane Dujarric akizungumza katika mkutano wa kila siku na waandishi wa habari kwa njia ya video jijini New York, Marekani, amemnukuu Katibu Mkuu akiendelea kusema kuwa, “Balozi Mahiga alikuwa mtumishi wa umma aliyekamilika na mwanadiplomasia aliyejizatiti na alishika wadhifa wa Mwakilishi Maalum wa Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa nchini Somalia kuanzia mwaka 2010 hadi 2013.”

Assumpta Massoi/UNNewsKiswahili
UNGA73-Balozi Agustine Mahiga, Tanzania

Amefafanua kuwa, “wakati akihudumu kwenye jukumu hilo, Balozi Mahiga alikuwa na dhima ya msingi katika kusongesha uundwaji wa serikali ya Somalia na kusaidia kukamilisha Katiba ya muda na maandalizi ya uchaguzi.”

Kando mwa kumwakilisha Katibu Mkuu huko Somalia, Balozi Mahiga alikuwa Mwakilishi wa Kudumu wa Tanzania kwenye Umoja wa Mataifa kuanzia mwaka 2003 hadi mwaka 2010.

Hadi mauti yanamkuta, Dkt. Mahiga ambaye alikuwa na umri wa miaka 74, alikuwa Waziri wa Katiba na Mambo ya Sheria ambapo awali alikuwa Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki kuanzia mwaka 2015 hadi 2019.