Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Taliban yaunga mkono kampeni ya WHO ya chanjo ya polio

Mtoto akipatiwa chanjo ya Polio huko Kandahar, Kusini mwa Afghanistan (Maktaba)
© UNICEF/Frank Dejongh
Mtoto akipatiwa chanjo ya Polio huko Kandahar, Kusini mwa Afghanistan (Maktaba)

Taliban yaunga mkono kampeni ya WHO ya chanjo ya polio

Afya

Uamuzi wa uongozi wa Taliban wa kuunga mkono kampeni ya nyumba kwa nyumba ya chanjo dhidi ya polio nchini Afghanistan umekaribishwa na shirika la afya la Umoja wa Mataifa WHO na shirika la Umoja wa Mataifa la kuhudumia Watoto UNICEF.

Kampeni hiyo ya chanjo ambayo itaanza tarehe 8 Novemba, itakuwa ya kwanza kwa zaidi ya miaka mitatu kuwafikia watoto wote nchini Afghanistan. 

Hii ni pamoja na zaidi ya watoto milioni tatu katika maeneo ya nchi hiyo ambayo hapo awali walibaki nyuma bila kufikiwa na kampeni za chanjo dhidi ya ugonjwa huo wa kuambukiza, ambao unaweza kusababisha kupooza na kifo. 

Kampeni ya pili ya chanjo ya kitaifa itafanyika sanjari na harakati ya kitaifa ya chanjo ya polio ya Pakistan mwezi Desemba. "Tunajua kwamba dozi nyingi za matone ya chanjo ya polio hutoa kinga bora. Ufikiaji endelevu kwa watoto wote ni muhimu katika kutokomeza kabisa polio. Hii lazima ibaki kuwa kipaumbele cha juu”.  Amesema Dapeng Luo, Mwakilishi wa WHO nchini Afghanistan. 

Fursa isiyo ya kawaida 

Kukiwa na kisa kimoja tu cha ugonjwa wa polio mwitu iliyoripotiwa mwaka huu nchini Afghanistan, nchi hiyo ina fursa ya kipekee ya kutokomeza ugonjwa huo, limesema shirika la WHO. 

Shirika hilo limesisitiza kwamba kuanza tena kwa chanjo ya polio sasa, ni muhimu ili kuzuia kuibuka tena kwa polio ndani ya nchi hiyo na kupunguza hatari ya kuvuka mpakani mpakani na kimataifa. 

Dozi ya matone ya vitamini A pia inatatolewa kwa watoto wenye umri wa miezi 6 hadi 59, wakati wa kampeni ijayo. "Ili kutokomeza polio kabisa, kila mtoto katika kila kaya kote nchini Afghanistan lazima apatiwe chanjo, na kwa kushirikiana na washirika wetu, hili ndio tunakusudia kulifanya," amesema Hervé Ludovic De Lys, mwakilishi wa UNICEF nchini Afghanistan. 

Maelfu ya familia wameyahama makazi yao kutokana na machafuko Afghanistan
© UNICEF/Sayed Bidel
Maelfu ya familia wameyahama makazi yao kutokana na machafuko Afghanistan

Surua, na chanjo ya  COVID 

Mpango wa chanjo ya polio ni matokeo ya mazungumzo ya ngazi ya juu kati ya Umoja wa Mataifa na uongozi wa Taliban ili kukidhi haraka mahitaji ya kiafya ya watu nchini Afghanistan. 

Ili kupunguza hatari ya kuongezeka kwa magonjwa kwa jumla, na vifo, pande zote pia zimekubaliana juu ya hitaji la kuanza mara moja kampeni za chanjo ya ukambi na COVID-19

WHO imebainisha kwamba hii itakamilishwa na msaada wa mpango wa kutokomeza polio na shughuli za ufikiaji ambazo zitaanza kutoa chanjo zingine za kuokoa maisha kupitia mpango wa kitaifa wa chanjo. 
Kujitolea kwa pamoja 
 
"Uharaka ambao uongozi wa Taliban unataka kampeni ya polio iendelee, unaonyesha dhamira ya pamoja ya kudumisha mfumo wa afya na kuanzisha tena chanjo muhimu ili kuzuia milipuko zaidi ya magonjwa yanayoweza kuzuilika," amesema Dk Ahmed Al Mandhari, mkurugenzi wa WHO wa kanda ya Mediterania ya Mashariki. 

Hata hivyo, WHO imesisitiza kwamba mfumo mzima wa afya nchini humo unabaki katika hatari. 

Kuziba mapengo 

Shirika la Umoja wa Mataifa la Uhamiaji (IOM) linasema linajiandaa kuziba mapengo haraka ili kusaidia kuhakikisha kuwa mfumo wa huduma ya afya wa Afghanistan hauporomoki. 

Hivi sasa, timu za IOM saba kati ya nane za huduma ya afya ya kuhamahama (MHTs) zinafanya kazi katika majimbo manne ya mpakani.  

Msaada pia umepangwa kupanua wigo hadi Kabul, mkoa wa magharibi wa Ghor, na mikoa ya kaskazini ya Balk, Badakhshan na Badghis. 

Katika majimbo haya ya kaskazini, IOM imesema inaongeza nguvu kusaidia idara ya afya ya umma ya mkoa na MHTs, timu za mwitikio wa haraka (RRTs) za COVID-19 na za chanjo za ziada. 

Usalama ndio nguzo 

WHO ilisisitiza kuwa ulinzi na usalama wa wafanyikazi wa afya unabaki kuwa wasiwasi mkubwa kwa mpango huo wa chanjo ya polio. 

Uongozi wa Taliban umeelezea kujitolea kwao kwa kujumuisha wafanyikazi wanawake wa mstitari wa mbele na kuhakikisha usalama wa wafanyikazi wote wa afya kote nchini, limesema shirika hilo. 

WHO na UNICEF wametoa wito kwa mamlaka na viongozi wa jamii katika ngazi zote kuheshimu na kudumisha mshikamano kwa hatua zote za kiafya, na kuhakikisha ufikiaji wa watoto wote bila vikwazo sasa na na siku za usoni.