Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

IOM yaomba wadau kuchangia dola milioni 15 kuisaidia Haiti

Msaada wa chakula unasambazwa kwa watu 3,000 walioko katika kambi ya Perrin baada ya kuathirika na tetemeko pamoja na Kimbunga Grace Kusini mwa nchi ya Haiti
© WFP/Marianela González
Msaada wa chakula unasambazwa kwa watu 3,000 walioko katika kambi ya Perrin baada ya kuathirika na tetemeko pamoja na Kimbunga Grace Kusini mwa nchi ya Haiti

IOM yaomba wadau kuchangia dola milioni 15 kuisaidia Haiti

Msaada wa Kibinadamu

Shirika la Umoja wa Mataifa la Uhamiaji IOM limezindua ombi maalum la kukusanya dola milioni 15 kwa ajili ya kusaidia uongozi wa nchi ya Haiti kwenye suala la makazi ya muda, msaada wa afya ya akili na kinga dhidi ya COVID-19 kwa familia zaidi ya 137,000 zilizoathiriwa na tetemeko la ardhi lililotokea kusini mwa nchi hiyo .

Naibu mwakilishi wa IOM nchini Haiti Federica Cecchet amesema takwimu za mpaka sasa zinaonesha watu waliokufa kutokana na tetemeko hilo ni 2,207, zaidi ya watu 12,000 wamejeruhiwa, karibu majengo 53,000 yameanguka, na mengine 77,000 wameharibiwa vibaya.

"Kwa kwezi huu wa kwanza pekee, tunahitaji angalau dola milioni 15 ili tuweze kutoa msaada wa makazi, kusaidia Wahaiti walioathiriwa kurudi nyumbani, na kuhakikisha wana njia muhimu za kujikimu ," amesema Cecchet.

Naibu mwakilishi huyo wa IOM amesema kiasi hicho cha fedha kinahitajika baada ya ofisi yao kufanya tathmini kwa kuweka vituo katika kila eneo lililoathiriwa ili kuweza kupata picha kamili ya uharibifu.

“Tunatumia picha za setelaiti kufanya uchambuzi na kutathmini uharibifu uliotokea kwa maelfu ya watu. Tuna timu ya wahandisi wanaosaidia kufanya tathmini ya kimuundo katika manispaa zilizoathiriwa kusini mwa Haiti.  Kwa sasa tumetoa makaratasi za plastiki kujikinga na mvua na kujifunika, vifaa vya usafi, blanketi, na vitu muhimu vya kutumia jikoni ili kuweza kusaidia kidogo familia zilizoathirika ziweze kuishi hata kama kwa hali duni.” 

 Msaada wa kisaikolojia

Majanga haya mawili ya tetemeko la ardhi na kimbunga Grace yameathiri watu kisaikolojia na tayari timu maalum  imejipanga kusaidia eneo hilo. 

“Tunakusudia kutoa huduma ya afya ya akili na msaada wa kisaikolojia kwa familia zilizoathirika, katika msaada huu tutazingatia zaidi wanawake na wasichana, kupitia wanasaikolojia wetu walioko maeneo hayo. Wanasaikolojia wa IOM wamepata mafunzo mazuri jinsi ya kusaidia waathirika wa unyanyasaji wa kijinsia na kingono na tutawalenga walioathiriwa na tetemeko la ardhi. Kwawale ambao hatutaweza kuwafikia moja kwa moja kuwapatiaa msaada huu  tumeweka namba maalum ya siku ya bure ya 840, kupitia namba hii pamoja na mambo mengine wataweza kupata msaada wa kisaikolojia, kupata taarifa mbalimbali na kutoa malalamiko yao."

Hospitali ya Imaculate iliyoko Les Cayes nchini Haiti imeathiriwa vibaya na tetemeko la ardhi la ukubwa wa richer 7.2 lililoikumba nchi hiyo
UNOCHA/Matteo Minasi
Hospitali ya Imaculate iliyoko Les Cayes nchini Haiti imeathiriwa vibaya na tetemeko la ardhi la ukubwa wa richer 7.2 lililoikumba nchi hiyo

 Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa

Katika hatua nyingine , wajumbe wa Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa hii leo mjini New York Marekani wanajadili hali ya misaada ya kibinadamu inavyoendelea  nchini Haiti.

Mwakilishi maalum na mkuu wa Ofisi ya Umoja wa Mataifa nchini Haiti Helen La Lime na na msaidizi wa Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa katika masuala ya Kibinadamu Martin Griffiths wanahudhuria kikao hicho. 

Nchi ya Haiti imekumbwa na majanga mawili siku za hivi karbuni ambapo ilipigwa na tetemeko la ardhi lenye ukubwa wa vipimo vya richer 7.2 mnamo 14 Agosti na kimbunga Grace mnamo 16 na 17 Agosti mwaka huu wa 2021. 

TAGS: IOM, Haiti, Baraza la Usalama, Misaada ya kibinadamu