Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Majanga yaliyowapata wananchi wa Haiti ni fursa ya kuanza upya: Amina Mohamed

Naibu Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Amina Mohammed ametembelea eneo la Les Cayes nchini Haiti baada ya kutokea tetemeko la ardhi
UNOCHA/Matteo Minasi
Naibu Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Amina Mohammed ametembelea eneo la Les Cayes nchini Haiti baada ya kutokea tetemeko la ardhi

Majanga yaliyowapata wananchi wa Haiti ni fursa ya kuanza upya: Amina Mohamed

Msaada wa Kibinadamu

Naibu katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Amina Mohammed amefanya ziara ya kikazi ya siku mbili nchini Haiti na kusema msaada wanaoupata nchi hiyo baada ya kukumbwa na majanga ya tetemeko la ardhi unatoa fursa kwao kuunda mshikamano mkubwa wa kitaifa na kupanga njia mpya ya kusonga mbele.

Akizungumza na waandishi wa habari mjini Port-au- prince, Bi Mohammed amesema idadi ya watu waliokufa baada ya tetemeko tarehe 14 Agost inazidi kuongezeka na mpaka sasa zaidi ya watu 2100 wameripotiwa kufa na majeruhi ni zaidi ya 10,000. 

Tetemeko la ardhi lilifuatiwa na kimbunga Grace ambacho kilisababisha mafuriko katika maeneo yaliyoathiriwa na tetemeko. Inakadiriwa watu 600,000 wanahitaji msaada wa kibinadamu.

Katika ziara hiyo Bi. Mohammed amekutana na jamii zilizoathirika na tetemeko katika mji wa Les Cayes. “ kwa mara nyingine tena naona uimara wa watu wa Haiti ambao wameteseka kwa kiasi kikubwa na wamehamasishana kusaidia majirani zao na jamii baada ya maafa ya tetemeko.”

Tarehe 19 Agost, Naibu Katibu huyo wa Umoja wa Mataifa alikutana na waziri mkuu wa Haiti Ariel Henry na wawakilishi wa asasi za kiraia na kupongeza serikali kwa juhudi walizofanya . “Binafsi nimevutiwa zaidi na kazi iliyofanywa na wakala wa kuwalinda raia wa Haiti – COUN, ambayo lazima iwezeshwe ili iweze kusimamia shughuli ya kuwasaidia waathirika.”

Katika mkutano huo na wanahabari Bi.Mohammed amewahakikishia wananchi wa Haiti kuwa umoja wa mataifa utaendelea kufanya kazi na uongozi wa serikali kuu na wilaya kuwasaidia sio tuu kuwapatia msaada sasa hivi wa baada ya majanga yaliyowakumba bali itawasaidia katika mchakato wa ujenzi upya. 

Amesema kwa kutumia tetemeko lililotokea mwaka 2010 kuna mambo kadhaa yakujifunza na kufanya tofauti ili Haiti iweze kurejea vyema zaidi. “tunatakiwa kuwekeza kwenye maendeleo ya muda mrefu na kusaidia uongozi wa serikali.”

Naye Mkuu wa Shirika la Mpango wa Maendeleo la Umoja wa Mataifa UNDP Achim Steiner alikuweko kwenye ziara hiyo na kusema” vitu nilivyoona kwenye ziara hii vinahuzunisha- kuna uharibifu mkubwa na maumivu. Na bado nimeona mshikamano mkubwa na matumaini ya watu wa Haiti wakati huu wanakabiliwa na majanga.  Nimefurahishwa sana na namna jamii zilivyojipanga kusaidia majirani zao na jamii nzima inavyowalinda watoa huduma walio mstari wa mbele  na watu wanaojitolea. UNDP itafanya kila iwezako kusaidia watu wa Haiti katika nyakati hizi na baadae wakati wa ujenzi upya.”