Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

UN yatoa milioni 8 kusaidia nchi ya Haiti

Kijana akiwa amesimama nje ya magofu ya mijengo nchini Haiti kufuatia tetemeko la ardhi na kimbunga Grace.
UNICEF/Georges Harry Rouzier
Kijana akiwa amesimama nje ya magofu ya mijengo nchini Haiti kufuatia tetemeko la ardhi na kimbunga Grace.

UN yatoa milioni 8 kusaidia nchi ya Haiti

Msaada wa Kibinadamu

Shirikia la Umoja wa Mataifa la kuhudumia watoto UNICEF nchini Haiti linakadiria watu milioni 1.2, wakiwemo watoto 540,000, wameathiriwa na tetemeko la ardhi na karibu watoto laki 5 hawana huduma ya malazi, maji safi na salama, pamoja na huduma za afya na lishe. Umoja wa Mataifa umetoa Dola Milioni 8 kuisadia nchi hiyo.

Nchi ya Haiti, kisiwa kidogo kilichoko ukanda wa Caribbea ndani ya wiki moja kimekumbwa na majanga makubwa mawili. Mosi Tetemeko la Ardhi liliotokea siku ya jumamosi na kuua takriban watu 2,000, kujeruhi watu 9,900  na kuharibu zaidi ya nyumba 115,000.

Jumatatu, ndani ya saa 48 baada ya tetemeko kikaja kimbunga Grace, ambacho pamoja na uharibifu mwingine, Shulle 94 zimesambaratishwa kabisa ikiwa ni wiki tatu tuu kabla wanafunzi kurejea shuleni hapo (Septemba 7, 2021).

Shirika la UNICEF, limebainisha zaidi ya watu Milioni 1.2 hawana huduma muhimu na tayari wameanza juhudi za kuwasaidia wa Haiti, na Mjini New York nchini Marekani kuhusu hilo Msemaji wa Umoja wa Mataifa Stephaane Dujarric amesema,"UMoja wa Mataifa umetenga dola milioni 8 kutoka Mfuko wa dharura ili kutoa huduma muhimu za afya, maji safi, makao ya dharura na usafi wa mazingira kwa watu wote walioathiriwa."

Majanga haya yameleta simanzi kubwa na msemaji huyu anawafikishia ujumbe wa faraja wathirika,“Katibu Mkuu wa UMoja wa Mataifa António Guterres amesema kuwa anasimama nanyi katika umoja na watu wa Haiti wakati huu mgumu mnaopitia, "ujumbe wake kwa watu wote wa Haiti ni kuwa, hampo pekeyenu. Tutasimama nanyi na kuwaunga mkono katika kila hatua kutokana na majanga haya “

Umoja wa Mataifa umewasihi nchi wanachama kushiriki kusaidia wananchi wa Haiti.

Majanga yote haya yanatokea ikiwa ni mwezi mmoja tuu tangu rais wa Haiti kuuwawa katika ikulu ya nchi hiyo Julai 07, mwaka huu wa 2021.