Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Wahudumu wa kibinadamu wahatarisha maisha yako kila uchao kuokoa ya wengine:Guterres 

Abel Cosaa mfanyakazi wa kibinadamu kutoka WFP akisaidia katika usambazaji wa msaada.
WFP/Rafael Campos
Abel Cosaa mfanyakazi wa kibinadamu kutoka WFP akisaidia katika usambazaji wa msaada.

Wahudumu wa kibinadamu wahatarisha maisha yako kila uchao kuokoa ya wengine:Guterres 

Msaada wa Kibinadamu

Leo ni siku ya wahudumu wa masuala ya kibinadamu duniani ambao wako msitari wa mbele kusaidia kuokoa maisha ya watu walio hatarini zaidi duniani majanga yanapozuka, na kwa kufanya hivyo huweka rehani maisha yao kila uchao amesema Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifaifa Antonio Guterres.

Kupitia ujumbe wake kwa ajili ya siku hii Guterres amesema kote duniani wahudumu wa kibinadamu wanakabiliwa na ongezeko la vitisho, Nas katika miaka 20 iliyopita matukio ya kupigwa risasi, kutekwa na mashambulizi mengine dhidi ya mashirika ya kibinadamu yameongezeka mara 10. 

Ameongeza kuwa mwaka huu pekee angalau wahudumu wa masuala ya kibinadamu 72 wameuawa katika maeneo ya mizozo, na kwa mantiki hiyo amesisitiza,“Katika siku hii ya wahudumu wa masuala ya kibinadamu tunawaenzi wahudumu hao kila kona ya dunia na kuahidi kufanya kila liwezekanalo kuwalinda wao na kazi yao muhimu.” 

Maudhui na kampeni kubwa ya siku ya mwaka huu imejikita katika mgogoro wa mabadiliko ya tabianchi ambao unatishia kusambaratisha nyumba, uwezo wa watu kuishi na maisha yao miongoni mwa watu masikini kabisa duniani. 

Katibu mkuu anamtaka kila mtu kujiunga na kampeni hiyo #TheHumanRace ili kusaidia kufikisha ujumbe kwa viongozi wa dunia kwamba hatua dhidi ya mabadiliko ya tabianchi hazitomwacha yeyote nyuma. 

Hivyo Guterres ameihimiza dunia kwamba,“Dharura ya mabadiliko ya tabianchi ni mbio tunazopoteza. Lakini ni mbio tunazoziweza na lazima tushinde. Hebu tukaze buti zetu zetu za kukimbilia, jiunge na Kampeni ya TheHumanRace, na kwa pamoja, hakikisha kila mtu anakamilisha mbio hizo.”