Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Wahudumu wa kibinadamu waendelea kuuawa kila  uchao- Guterres

Wahudumu wa misaada wakiandaa chakula kwa ajili ya wasomali kwenye moja ya kituo cha lishe kinachopatiwa msaada na WFP huko Mogadishu, Somalia
OCHA/A. Gaitanis
Wahudumu wa misaada wakiandaa chakula kwa ajili ya wasomali kwenye moja ya kituo cha lishe kinachopatiwa msaada na WFP huko Mogadishu, Somalia

Wahudumu wa kibinadamu waendelea kuuawa kila  uchao- Guterres

Msaada wa Kibinadamu

Hii leo ni siku ya kimataifa ya usaidizi wa kibinadamu ambapo Umoja wa Mataifa unatoa wito kwa viongozi ulimwenguni kufanya kila wawezalo kulinda watu walionasa kwenye mizozo.

Kupitia ujumbe wake, Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterres anasema hatua hiyo ni muhimu kwa kuwa mizozo inaongezeka,raia wanaolengwa kwenye mizozo vivyo  hivyo, halikadhalika wale wanaofunga safari kwenda kuwasaidia.

Ametolea mfano kuwa miaka 15 tangu shambulio dhidi ya ofisi za Umoja wa Mataifa huko Baghdad nchini Iraq lililosababisha vifo vya wafanyakazi 22, idadi ya wafanyakazi waliouawa, kujeruhiwa au kushikiliwa wakiwa kazini ni zaidi ya 4000.

“Kiwango hicho kinamaanisha kuwa wastani wa wafanyakazi 300 wa kutoa huduma za misaada wanauawa kila mwaka,” amesema Katibu Mkuu.

Guterres amesema raia nao hawako salama kwani kwenye maeneo  ya mizozo, wanauawa, wanauawa au kuachwa na  ulemavu katika mashambulizi ya makusudi au yasiyochagua popote.

Majeruhi wa tetemeko la arshi la Agosti 5, 2018 Lombok Kaskazini anahamishwa na wafanyakazi wa msalaba mwekundu.
Indonesian Red Cross
Majeruhi wa tetemeko la arshi la Agosti 5, 2018 Lombok Kaskazini anahamishwa na wafanyakazi wa msalaba mwekundu.

“Mwaka jana, Umoja wa Mataifa ulibaini kuwa zaidi ya raia 26,000 waliuawa kwenye mapigano katika nchi sita pekee ambazo ni Afghanistan, Jamhuri ya Afrika ya Kati, Jamhuri ya kidemokrasia ya Congo, DRC, Iraq, Somalia na Yemen,” amesema Bwana Guterres katika ujumbe wake uliopo pia kwa njia ya video.

Ni kutokana na mapigano hayo, amesema Katibu Mkuu, ulimwenguni kote idadi ya watu waliofurushwa makwao ni zaidi ya milioni 65, watoto nao wakitumikishwa vitani.

Kwa mantiki hiyo Katibu mkuu anatoa wito kwa wote wanaohusiak kuungana katika kampeni ya siku ya usaidizi wa kibinadamu hii leo kupitia wavuti www.worldhumanitarianday.org na kuonyesha mshikamano kuwa raia si walenga. #SiMlengwa, #NotATarget

“Sote kwa pamoja, tushikamane na raia walioko kwenye mzozo, na wafanyakazi wa huduma za misaada ambao wanaweka maisha yao hatarini ili kuwasaidia,” amehitimisha Katibu Mkuu.

Siku ya kimataifa ya wafanyakazi wa kibinadamu ilianzishwa na Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa mwaka 2008 kuenzi watendaji wa chombo hicho waliouawa wakati wa mashambulizi dhidi ya makao makuu ya UN huko Baghdad, Iraq mwaka 2005.