Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Wahudumu wa kibinadamu ni wa kwanza kuwasIli na wa mwisho kuondoka kwenye kila janga- Profesa Tijjani-Bande

Wahudumu wa afya wakitoa matibabu kwa mtoto wa umri wa miaka 15 ambaye anashukiwa kuugua Ebola nchini Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo, DRC.
World Bank/Vincent Tremeau
Wahudumu wa afya wakitoa matibabu kwa mtoto wa umri wa miaka 15 ambaye anashukiwa kuugua Ebola nchini Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo, DRC.

Wahudumu wa kibinadamu ni wa kwanza kuwasIli na wa mwisho kuondoka kwenye kila janga- Profesa Tijjani-Bande

Msaada wa Kibinadamu

Wahudumu wa kibinadamu ni wanawake na wanaume mashujaa ambao hufikisha msaada wa kuokoa maisha kama malazi, huduma muhimu za afya, chakula, maji na huduma za usafi kwa watu wasiojiweza na walio hatarini, hivyo wanastahili kuheshimiwa na kupongezwa. 

 

Hiyo ni kauli ya Rais wa Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa Tijjani Muhammad-Bande katika ujumbe wake maalum kwa ajili ya siku ya huduma za kibinadamu duniani ambayo kila mwaka huadhimishwa Agosti 19. 

Bwana Bande amesema wahudumu hao wa kibinadamu na wafanyakazi walio msitari wa mbele , wanawasaidia watu na jamii katika vita dhidi ya umasikini , kutokuwepo na haki na kupoteza matumaini huku wakilinda haki za msingi za binadamu za watu waliotawanywa na vita na migogoro. 

Ameongeza kuwa “Ni watu wa kwanza kuwasili kuchukua hatua na wa mwisho kuondoka, wakiikubali hatari ya kutishiwa, kujeruhiwa, kutekwa na kuuawa. Ukatili dhidi ya wahudumu wa misaada ya kibinadamu imekuwa hofu kubwa kwa mashirika ya kibinadamu na wakati huohuo hali ya kuzingatia sheria za kimataifa za kibinadamu inaendelea kuzorota.” 

Rais huyo wa Baraza Kuu amesema mwaka 2019 kulikuwa na mashambulizi 483 dhidi ya wahudumu wa kibinadamu ikiwa ni idadi kubwa zaidi kuwahi kurekodiwa. 

Amesisitiza kuwa “Mahitaji ya kimataifa ya kibinadamu bado ni makubwa, na migogoro mingi ya kibinadamu inaendelea au kuwa mibaya zaidi iwe ni katika hali ya vita au kutokana na majanga ya asili.” 

Akienzi kujitolea kwa wahudumu hao wa kibinadamu Bande amesema “Mwaka 2020, licha ya kuwa na pengo kubwa la ufadhili wahudumu wa kibinadamu wamekabiliwa na janga kubwa la COVID-19, pamoja na ongezeko la mahitaji ya kibinadamu katika nchi 63. Wakati dunia ikipambana na janga hilo tunawaenzi wahudumu waliopoteza maisha wakitoa huduma za kibinadamu.” 

Amesema janga la hivi karibuni la Lebanon ni mfano dhahiri wa ongezeko la mahitaji ya msaada wa kibinadamu hususan kwa watu walio hatarini zaidi, na picha za kutisha kutoka mjini Beirut ni kumbusho kwamba msaada wa kibinadamu unapaswa kusalia kuwa kitovu cha mchakato wa kimataifa wa kutoa huduma za kibinadamu. 

Zaidi ya hapo Rais wa Baraza kuu amesema “wanawake, wasichana na watoto wanasalia kuwa miongoni mwa makundi yaliyo hatarini na lazima kila wakati wapewe kipaumbele katika masuala ya msaada. Tunapaswa kutumia siku hii kutafakari ni vipi tunaweza kufanyakazi vyema Pamoja , kuiokoa dunia katika hatua mabazo zinatuweka sote katika maafa.” 

Na kwa mantiki hiyo amesema “Leo tunawaangazia wahudumu wa kibinadamu ambao wanaendelea kusaidia watu walio hatarini katika mazingira magumu, asanteni sana kwa juhudi zenu za bila kuchoka na kwa utu wenu, nyie ni mashujaa wa kweli.”