Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Muafaka wa muda wa amani umeleta afueni Yemen tunaomba uendelee:OHCHR 

Watoto katika kipindi cha kusoma katika kituo cha wakimbizi Ta'iziyah, Yemen.
IOM/Olivia Headon
Watoto katika kipindi cha kusoma katika kituo cha wakimbizi Ta'iziyah, Yemen.

Muafaka wa muda wa amani umeleta afueni Yemen tunaomba uendelee:OHCHR 

Msaada wa Kibinadamu

Ofisi ya haki za binadamu ya Umoja wa Mataifa OHCHR imesema leo kwamba muafaka wa usitishaji uhasama kwa muda nchini Yemen umeleta afueni kwa mamilioni ya Wayemen na imetaka hali hiyo iendelee. 

Akizungumza na waandishi wa Habari mjini Geneva Uswis msemaji wa OHCHR Liz Throssell amesema “Tumeeleza mara kwa mara kuhusu athari mbaya ambazo vita nchini Yemen, iliyoanza mwaka wa 2015, imekuwa nazo kwa raia. Lakini kwa muda wa miezi miwili iliyopita, mapatano ya amani yamemaanisha kuwa watu wa Yemen wameshuhudia ghasia na uhasama vikipungua.” 

Kwa hiyo amesema ofisi hiyo inakaribisha  hatua ya kukubali kuongezwa muda wa muafaka huo wa amani kwa miezi miwili zaidi kutoka kwa pande zote zinazohusika katika mzozo huo ambazo ni serikali inayotambuliwa kimataifa inayoungwa mkono na muungano unaoongozwa na Saudi Arabia, na vuguvugu la Ansar Allah  

Kati ya tarehe 2 Aprili na 1 Juni, Ofisi ya Haki za binadamu ya Umoja wa Mataifa nchini Yemen, ikiwa ni sehemu ya kazi yake inayoendelea ya ufuatiliaji na kuweka kumbukumbu za vifo vya raia, ilikusanya taarifa za awali zinazoonyesha kuwa takriban raia 19 waliuawa na 32 kujeruhiwa katika baadhi ya matukio 20 ya machafuko yanayohusiana na migogoro unaoendelea Yemen. 

Mabomu ya kutegwa ardhini ni hatari kubwa 

Kwa mujibu wa ofisi hiyo ya haki za binadamu wengi wa majeruhi hawa wametokana na mabomu ya kutegwa ardhini, ikiwa ni pamoja na mabaki ya vifaa vingine vya milipuko ya vita.  

“Hii inasisitiza tishio la vifaa hivi kwa raia, mara nyingi na kwa muda mrefu, na husababisha vifo au majeraha makubwa. Watoto wako katika hatari zaidi. Tangu tarehe 2 Aprili hadi Juni 1, watoto watatu waliripotiwa kuuawa na wengine 12 kujeruhiwa kwa njia hii.” 

Kwa kuzingatia kuenea kwa matumizi ya mabomu ya kutegwa ardhini, licha ya athari zake kiholela, na uwepo wa silaha zisizolipuka, haswa huko Hudaydah, hali hii kwa bahati mbaya inatarajiwa kuendelea huku watu wakiingia kwenye maeneo yaliyoathirika.  

“Tunazihimiza pande zote katika mzozo kushirikiana na, na kutoa fursa ya ufikiaji kamili na salama wa maeneo hayo kwa, timu za wasaidizi wa kibinadamu ambao ni wateguaji wa mabomu. Pia tunatoa wito kwa wahusika wote wa kikanda na kimataifa wanaohusika katika mzozo wa Yemen kuhakikisha kwamba shughuli za utegaji mabomu na shughuli za uhamasishaji kuhusu hatari za mabomu hayo hasa mashuleni, zinafadhiliwa vya kutosha.” 

Pamoja na maafikiano hayo, Ofisi ya haki za binadamu ilirekodi matukio manne ya kupigwa risasi na wavamizi na kusababisha mauaji ya raia watatu akiwemo mwanamke mmoja na kujeruhi vibaya raia wawili akiwemo mtoto wa kiume katika maeneo yanayodhibitiwa na Serikali karibu na mstari wa mbele kwenye majimbo ya Al Dalee na Ta'izz. 

Matukio mawili pia yalirekodiwa ambapo silaha zilizorushwa kutoka kwa ndege zisizo na rubani zilijeruhi raia wanne, akiwemo msichana tena katika maeneo yanayodhibitiwa na serikali karibu na mstari wa mbele wa mapambano. 

Pande zote lazima zihakikishe barabra zinafunguliwa 

OHCHR imezitaka pande husika katika mzozo kufanya juhudi za dhati kuhakikisha kuwa barabara za kuingia katika jiji la Ta’izz zinafunguliwa tena. Ta’izz kimsingi imekuwa ikizingirwa na Ansar Allah tangu mwaka 2015.  

Kuna hali mbaya ya kibinadamu yhuko hivi sasa, watu wanakabiliwa na changamoto kubwa katika kupata maji, kununua chakula na kupata huduma za matibabu.  

Ofisi hiyo imeongeza kuwa watu wengi Ta’izz, kama ilivyo katika maeneo mengine ya Yemen, wamepata kiwewe kikubwa wakati wa mzozo kutokana na viwango vya juu vya ghasia za kutumia silaha, na ukiukwaji wa sheria za kimataifa za kibinadamu na haki za binadamu, ikiwa ni pamoja na mashambulizi yanayolenga raia. 

 Pia kuna ripoti kwamba wahusika kwenye mzozo wanaweza kujipanga tena ikiwa operesheni za kijeshi zitaanza tena.  

“Tunatoa wito kwao kuzingatia masharti ya mapatano hayo kwa nia njema na kujiepusha kabisa na kampeni za kuajiri zinazolenga kuwaleta watoto katika vyeo vyao  vya kijeshi kitendo ambacho ni kinyume cha sheria ambacho kinakiuka ahadi zilizotolewa na pande zote.” 

Ofisi ya Haki za Kibinadamu itaendelea kufuatilia na kuorodhesha madhara yanayosababishwa kwa raia kutokana na ghasia zinazohusiana na migogoro na ukiukwaji wa haki za binadamu na sheria za kimataifa za kibinadamu.