Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Tusisubiri baa la njaa litangazwe ndio tuisaidie Somalia: FAO

Familia za Wasomali zilikimbia makazi yao huko Dhobley karibu na mpaka wa Somalia na Kenya.
FAO Somalia
Familia za Wasomali zilikimbia makazi yao huko Dhobley karibu na mpaka wa Somalia na Kenya.

Tusisubiri baa la njaa litangazwe ndio tuisaidie Somalia: FAO

Msaada wa Kibinadamu

Shirika la Umoja wa Mataifa la Chakula na Kilimo FAO nchini Somalia limetoa ombi la dola milioni 131.4 ili kusaidia wananchi 882,000 kutoka wilaya 55 wenye uhitaji wa haraka wa msaada wa kuokoa maisha yao. FAO wameisihi jumuiya ya kimataifa kutosubiri mpaka nchi hiyo itangaze kuwa na baa la ndio hatua zichukuliwe na badala yake wameomba hatua kuchukuliwa sasa.

Uti wa mgongo wa taifa la Somalia ni kilimo kinachotegemewa kwa takriban asilimia 60 kuendesha Maisha ya wananchi waweze kujipatia chakula na kile wanachouza waweze kujikimu, lakini mabadiliko ya tabianchi yaliyoleta ukame mkali nchini humo yamesababisha zaidi ya wananchi 900,000 wengi kutoka vijijini kuyakimbia makazi yao kusaka misaada katika kambi za wakimbizi wa ndani tangu mwezi Januari mwaka jana 2021 ili angalau waweze kupata chakula na kuweza kuishi. 

Mkurugenzi wa FAO anayehusika na dharura na mnepo Rein Paulsen hivi karibuni ametembelea nchini humo kujionea hali halisi na pia kuzungumza na wakimbizi wa ndani walio katika makambi ambao wengine wamemueleza mifugo yao imekufa sababu ya ukame na kutembea zaidi ya kilometa 100 kutafuta msaada kambini hapo.

Paulsen amesema ili kutatua changamoto nchini Somalia lazima kuanza kutibu kwenye mzizi wa tatizo “Mwitikio wa tatizo la njaa uanzie maeneo ya vijijini, huko ndio kwenye kitovu cha tatizo ambapo jumuiya za wazalishaji wa chakula wameathirika na ukame mkali. Hatuwezi kusubiri mpaka njaa itangazwe, lazima tuchukue hatua sasa ili kusaidia watu kupata riziki na kuweza kuishi.”

Akizungumzia kuhusu muitikio wa watu kuchangia misaadda ya kibinadamu amesema “Ufadhili umeendelea kuwa mdogo mpaka kufikia jana Agosti 4,2022 ni asilimia 43 pekee ya ufadhili imepatika.” Hii ikiwa sawa na asilimia 46 ya ufadhili unaohitajika nchini Somalia.

Safiya Mahdi Cise, mnufaika wa mradi wa FAO wa kuboresha ufugaji akiwa amembeba ndama wa kondoo huko kijiji cha  Duudwayne, wilaya ya Baki nchini Somalia
© FAO / Isak Amin / Arete
Safiya Mahdi Cise, mnufaika wa mradi wa FAO wa kuboresha ufugaji akiwa amembeba ndama wa kondoo huko kijiji cha Duudwayne, wilaya ya Baki nchini Somalia

Mkurugenzi huyo wa dharura wa FAO amesema kwa ufadhili waliopata mpaka sasa wameweka nguvu zaidi katika kutoa fedha taslimu ili watu waweze kununua chakula na kujikimu, kulisha mifugo yao, kuwapatia maji safi na salama na kupatia matibabu mifugo yao. “Licha ya changamoto ya uhaba wa mvua, tunahakikisha tunafikisha msaada kwa wakulima ili waweze kupanda pale inapowezekana, kilimo cha umwagiliaji kinawezekana. Hizi ndio aina za misaada ya vitendo inayohitajika”. 

FAO nchini Somalia imetoa ombi hilo la dola milioni 131.4 lengo kuu ni kuongeza utoaji wa misaada vijijini ili kuwasaidia watu wasiojiweza pale walipo. “Huu ni ufanisi zaidi, ni ubinadamu zaidi na nilazima kwa pamoja tuongeze juhudi kwakuwa kiwango cha msaada kilichotolewa sasa hakitoshi kwahiyo tunahitaji mwitikio wa msaada kutoka katika kila sekta ili kusaidia maisha ya watu."