Mapenzi ya ufumaji yampa riziki Libya mkimbizi kutoka Syria

17 Agosti 2021

Kutana na mkimbizi Fidaa kutoka Syria ambaye pamoja na familia yake walifungasha virago miaka minane iliyopita wakikimbia mapigano na kupata hifadhi Libya. Sasa changamoto za janga la corona au COVID-19 zimemlazimisha kurejea mapenzi ya zamani ya ufumaji ili kupata mkate wa kila siku wa familia yake.

Fidaa akiwa katika maskani yake mapya ukimbizini Libya anakumbuka kwamba kufuma kwake haikuwa kwa ajili ya kumudu maisha bali kwa ajili ya mapenzi kwani yeye na familia yake walijitosheleza kwa kila hali  Syria wanamiliki nyumba na kuishi maisha yaraha. 

Lakini sasa mama huyo mwenye umri wa miaka 42 hana jinsi bali kugeuza mapenzi ya ufumaji kuwa chanzo cha kipato ili kukimu mahitaji ya familia yake. Na anafuma na kuuza vitu mbalimbali kama anavyoeleza “Ninafuma magauni kwa ajili ya wasichana kwa kutumia uzi wa sweta, nafuma mablanketi, soksi, kofia, vibanio vya nywele na kitu kingine chochote kitakachoniingizia kipato.” 

Walipowasili Libya mumewe aitwaye Hani ndiye aliyekuwa akiendesha familia kwani aliweza kufanya kazi mbalimbali za mikono ili kumtunza mkewe na watoto wao wawili wa kike Ghazali na Mariam, lakini janga la corona au COVID-19 lilipozuka kitumbua kikaingia mchanga, kupata kazi ikawa tabu na afya yake ikaanza kuzorota ndipo Fidaa aipoamua kuvaa viatu vya mumewe kuinusuru familia yao. Hani anasema,“Alipoanza kufanyakazi ya ufumaji aliziba pengo la fedha tulilokuwanalo. Wakati tulipohitaji sahani nyumbani aliuza gauni na badala ya sahani moja alinunua tatu. Na alipouza kitu kingine alinunua sufuria za kupikia.” 

Wakimbizi kama Fidaa na Hani ni sehemu tu ya mamilioni ya wakimbizi wa Syria wanaohaha ukimbizini kwa miaka 10 sasa tangu mzozo kuzuka nchini mwao, na wengi wao wako Lebanon, Uturuki, Jordan, Libya na wengine kwa mamilioni wakisalia wakimbizi wa ndani nchini Syria. 

 

♦ Kutembelea ukurasa maalum wa COP26 bofya  hapa.
♦ Iwapo ungependa kupokea taarifa kutoka UN News Kiswahili kila wakati zinapochapishwa jisajili  hapa.
♦ Pia unaweza kupakua apu ili kusikiliza matangazo yetu wakati wowote popote ulipo.
♦ Tembelea pia chaneli yetu ya Youtube na pia Soundcloud na Twitter