UNHCR yafanikiwa kuwahamisha wakimbizi waliokuwa wakishikiliwa nchini Libya.

18 Oktoba 2018

Baada ya hali mbaya ya usalama kuongezeka mjini Tripoli, shirika la kuhudumia wakimbizi la Umoja wa Mataifa, UNHCR limefanikiwa kuwahamisha watu 135 kutoka Libya kuelekea Niger.

Taarifa ya shirika hilo iliyotolewa hii leo mjini Geneva, Uswisi,imesema idadi kubwa ya waliohamishwa ni wale waliokuwa wakishikiliwa kwa miezi kadhaa katika vituo na walikuwa wameathirika na utapiamlo na hali mbaya ya afya. Kwa sasa watu hao wanatunzwa na UNHCR kitengo cha dharura hadi pale suluhisho kwa ajili yao litakapopatikana.

 “Uhamisho huu ni wa kubadili na kuokoa maisha kwa wakimbizi waliokuwa wamekwama katika vituo hivyo nchini Libya na mara nyingi wanaokuwa waameshikiliwa wanaathirika na hali mbaya na wanakuwa hatarini kuuzwa” amesema Roberto Mignone mkuu wa UNHCR nchini Libya.

Taarifa hii imeeleza kuwa wafanyakazi wa UNHCR walipitia katika changamoto za vikwazo vya kiusalama na vizuizi hadi kukamilisha kazi ya kuwahamisha wakimbizi hao kutokana na mapigano kati ya pande zinazokinzana kiasi cha kusababisha mabomu mengine kudondoka katika uwanja wa ndege wa Tripoli.

Wafanyakazi wa UNHCR wakikitoa msaada kwa wakimbizi na waomba hifadhi baada ya mapigano kuibuka tena nchini Libya.
UNHCR/Sufyan Ararah
Wafanyakazi wa UNHCR wakikitoa msaada kwa wakimbizi na waomba hifadhi baada ya mapigano kuibuka tena nchini Libya.

 

Watu hao 135 waliookolewa ni wa kwanza kuhamishwa kutoka Libya tangu mwezi Juni mwaka huu ambapo UNHCR inasema kufanikiwa kuwahamisha wakimbizi hawa kunafanya idadi ya waliokolewa na kuhamishwa kutoka Libya kwa hisani ya UNHCR kufikia 1997 tangu shughuli ya kuhamisha watu ilipoanza mwaka 2017.

UNHCR imewashukuru viongozi wa Libya kwa kutoa mwanya wa kuwafikia wakimbizi hao na pia imeishukuru serikali ya Niger kwa mapokezi ya dharura.

Taarifa hii ya UNHCR imeongeza kuwa wakati uhamisho nchini Libya ukiendelea, pia wakimbizi 85 kutoka Syria, Sudan na Eritrea waliondoka Tripoli Libya kuelekea Timisoara Romania kwa msaada wa Shirika la Umoja wa Mataifa linalohusika na wahamiaji, IOM. 

Watu hao watasalia chini ya kitengo cha dharura cha UNHCR kabla ya kusafiri tena kuelekea nchini Norway.

 

♦ Kurambaza ukurasa mahsusi wa Siku ya Kiswahili Duniani bofya  hapa.
♦ Iwapo ungependa kupokea taarifa kutoka UN News Kiswahili kila wakati zinapochapishwa jisajili  hapa.
♦ Pia unaweza kupakua apu ili kusikiliza matangazo yetu wakati wowote popote ulipo.
♦ Tembelea pia chaneli yetu ya Youtube na pia Soundcloud na Twitter