Chondechonde Taliban jizuieni na machafuko zaidi kunusuru maisha ya watu:UN

16 Agosti 2021

Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa limekutana leo kwa dharura kujadili hali nchini Afghanistan ambako kundi la Taliban limepokonya mamlaka jana Jumapili baada ya vikosi vya serikali kuzidiwa nguvu na Rais ashraf Ghani kukimbilia ughaibuni. 

Taliban walivamia ikulu ya rais huko Kabul Jumapili jioni na matukio ya hofu na taharuki yalionekana katika uwanja wa ndege wa kimataifa katika mji mkuu wa Afghanistan, ambapo maelfu ya watu wanajaribu kukimbia. 

"Ulimwengu unafuatilia kinachoendelea huko Afghanistan kwa moyo mzito na wasiwasi mkubwa  hasa kwa juu ya nini kitafuata. Sote tumeona video katika wakati halisi. Machafuko, misukosuko, kutokuwa na uhakika, na hofu vikitawala” Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa António Guterres amewaambia wajumbe wa Baraza la Usalama. 

"Katika wakati huu wa madhila na mauti, ninahimiza pande zote, haswa Taliban, kujizuia kabisa ili kulinda maisha na kuhakikisha kuwa mahitaji ya kibinadamu yanaweza kutimizwa," akaongeza. 

Mkuu huyo wa Umoja wa Mataifa amekumbusha kwamba mzozo huo ulikuwa umelazimisha mamia ya maelfu ya watu kuondoka majumbani mwao na kwamba Kabul imeshuhudia utitiri mkubwa wa watu waliokimbia makazi yao. 

Guterres amezikumbusha pande zote katika mzozo juu ya wajibu wao wa kulinda raia na kuwataka wayape mashirika ya kibinadamu fursa ya kufika bila vizuizi ili kutoa huduma na msaada haraka kwa wanaouhitaji.  

Pia amezitaka nchi zote kukubali kupokea wakimbizi wa Afghanistan na kujiepusha na kuwafukuza. 

 Wito wa mshikamano 

Kutokana na hali ya mgogoro nchini Afghanistan, Katibu Mkuu ametoa wito kwa jamii ya kimataifa kushikamana na haswa "kuzungumza kwa kauli moja kutetea haki za binadamu" katika nchi hiyo. 

Katibu Mkuu ametoa wito kwa Taliban na pande zote kuheshimu na kulinda sheria za kimataifa za kibinadamu na haki na uhuru wa watu wote. 

Amelezea wasiwasi wake kutokanaa na"hadithi zinazoongezeka za ukiukaji wa haki za binadamu dhidi ya wanawake na wasichana nchini Afghanistan ambao wanaogopa kurejea katika siku zenye giza zaidi. Ni muhimu kwamba haki zilizopiganiwa kwa bidii za wanawake na wasichana wa Afghanistan zilindwe," ameongeza. 

Guterres pia ametoa wito kwa jamii ya kimataifa kuhakikisha kwamba Afghanistan haitumiwi tena kama jukwaa au kimbilio kwa mashirika ya kigaidi. 

"Natoa wito kwa Baraza la Usalama na jamii ya kimataifa kwa jumla kusimama katika mshikamano, kufanya kazi pamoja na kuchukua hatua kwa pamoja na kutumia nyenzo zote wanazoweza kukomesha tishio la kigaidi ulimwenguni na nchini Afghanistan na pia kuhakikisha uheshimuji wa haki za msingi za binadamu.” 

Watoto wakike wakiwa wamekusanyika katika kambi ya wakimbizi wa ndani Kandahar huko Kusini Magharibi mwa Afghanistan
© UNICEF Afghanistan
Watoto wakike wakiwa wamekusanyika katika kambi ya wakimbizi wa ndani Kandahar huko Kusini Magharibi mwa Afghanistan

 Haijalishi nani anashika hatamu haki lazima ziheshimiwe 

Katibu Mkuu amesisitiza kwamba "Haijalishi ni nani anashikilia madaraka, kanuni hizi mbili za msingi ambazo ulimwengu wetu una nia ya kina na ya kila wakati ya kuzitimiza lazima ziheshimiwe". 

Bwana Guterres amekumbusha kuwa Umoja wa Mataifa upo nchini humo na amefarijika kutangaza kwamba, kwa kiwango kikubwa, wafanyikazi na majengo ya Umoja wa Mataifa wameheshimiwa. "Tunaendelea kulisisitiza kundi la Taliban kuheshimu uadilifu wa vituo hivi na kutokushambuliwa kwa wajumbe wa kidiplomasia na majengo yao ," ameongeza. 

Kuhusu mgogoro wa kibinadamu nchini Afghanistan ambao unaathiri watu milioni 18, au nusu ya idadi ya watu wote nchini humo, amesema ni muhimu huduma za msingi ziendelee kutolewa. 

“Uwepo wa Umoja wa Mataifa utazingatia hali ya usalama. Lakini juu ya yote, tutakaa na kuunga mkono watu wa Afghanistan, "amesema, huku akitaka kukomeshwa kwa ghasia mara moja, kuheshimu haki za Waafghanistan wote na heshima ya Afghanistan kwa wote na pia mikataba ya kimataifa ambayo nchi hiyo ni mwanachama. 

 

♦ Kutembelea ukurasa maalum wa UNGA76 bofya  hapa.
♦ Iwapo ungependa kupokea taarifa kutoka UN News Kiswahili kila wakati zinapochapishwa jisajili  hapa.
♦ Pia unaweza kupakua apu ili kusikiliza matangazo yetu wakati wowote popote ulipo.
♦ Tembelea pia chaneli yetu ya Youtube na pia Soundcloud na Twitter