Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Hali bado ni tete Afghanistan licha ya ahadi za Taliban:UN

Umoja wa Mataifa umekuwa ukisaidia familia za wakimbizi wa ndani nchini Afghanistan, kuwapatia makazi na dharura na usalama
IOM/Mohammed Muse
Umoja wa Mataifa umekuwa ukisaidia familia za wakimbizi wa ndani nchini Afghanistan, kuwapatia makazi na dharura na usalama

Hali bado ni tete Afghanistan licha ya ahadi za Taliban:UN

Amani na Usalama

Mashirika ya Umoja wa Mataifa yanaendelea kufuatilia kwa karibu hali nchini Afghanistan na kusema bado ni tete licha ya ishara ndogo za matumaini hasa katika mji mkuu Kabul na ahadi zilizotolewa na kundi la Taliban kuwanusuru wananchi ambao kwa maelfu wanahaha kukimbia kwenda kusaka usalama. 

Kupitia taarifa yake iliyotolewa leo mjini Geneva Uswis , ofisi ya haki za binadamu ya Umoja wa Mataifa OHCHR imesema hali ya taharuki iliyoshuhudiwa jana kwenye uwanja wa ndege wa Kabul inasisitiza ukubwa wa tatitzo baada ya kundi la Taliban kushika usukani wa miji yote mikubwa yenye watu wengi nchini Afghanistan. 

Taarifa hiyo imeongeza kuwa “ Kwa bahati nzuri, mji mkuu na miji mingine mikubwa ya mwisho kutekwa kama Jalalabad na Mazar-e-Sharif haikukumbwa na mapigano ya muda mrefu, umwagaji damu au uharibifu. Walakini, hofu iliyotanda kwa idadi kubwa ya watu ni kubwa, na kulingana na historia ya zamani inaeleweka kabisa.” 


 Ahadi za Taliban kwa wananchi 

Ofisi hiyo ya haki za binadamu ya Umoja wa Mataifa imesema kufuatia hofu iliyopo kundi la Taliban limeaihi kuwapa haki wananchi “Wasemaji wa Taliban wametoa taarifa kadhaa katika siku za hivi karibuni, pamoja na kuahidi msamaha kwa wale ambao walifanya kazi kwa Serikali iliyopita. Wameahidi pia kuwa wajumuishi. Wamesema mwanamke anaweza kufanya kazi na wasichana wanaweza kwenda shule. Ahadi kama hizo zitahitaji kuheshimiwa, na hasa kwa wakati huu ukizingatia historia ya zamani, maazimio haya yamekaribishwa na wasiwasi. Walakini, ahadi hizo zimetolewa, na ikiwa zinaheshimiwa au zitavunjwa zitachunguzwa kwa karibu.” 

OHCHR imeongeza kuwa kumekuwa na maendeleo mengi yaliyopatikana kwa bidii katika haki za binadamu katika miongo miwili iliyopita hata hivyo imesisitiza kuwa haki za Waafghanistan wote zinapaswa kutetewa.  

“Tuna wasiwasi sana juu ya usalama wa maelfu ya Waafghan ambao wamekuwa wakifanya kazi kudumisha haki za binadamu kote nchini, na wamesaidia kuboresha maisha ya mamilioni ya watu.” 

Kwa mantyiki hiyo ofisi hiyo imetoa wito kwa jamii ya kimataifa kutoa msaada  kwa wale ambao wanaweza kuwa hatarini zaidi, na kutoa wito kwa Taliban kuonyesha kupitia matendo yao, sio tu maneno yao, kwamba hofu ya usalama wa watu wengi kutoka matabaka tofauti ya maisha unashughulikiwa. 

Mama na mtoto wake wakiume , ambao waliungua moto wakati nyumba yao iliposhambuliwa, wanaomba hifadhi katika kambi ya wakimbizi wa ndani ya Haji iliyoko Kandahar nchini Afghanistan
© UNICEF Afghanistan
Mama na mtoto wake wakiume , ambao waliungua moto wakati nyumba yao iliposhambuliwa, wanaomba hifadhi katika kambi ya wakimbizi wa ndani ya Haji iliyoko Kandahar nchini Afghanistan


 Mashirika mengine ya UN 


Mashirika mengine ya Umoja wa Mataifa yameendelea kushirikiana na kuwa karibu kufuatilia hali inayoendelea hasa kuhakikisha misaada ya kibinadamu ikiwemo matibabu, chakula na malazi inapatikana kwa wanaoihitaji zaidi. 

Kwa upande wake shirika la Umoja wa Mataifa la kuhudumia Watoto UNICEF kupitia mkuu wake wa shughuli na dharura, Mustapha Ben Messaoud, aliyezungumza leo mjini Geneva amesema "Hali inaboreka kiasi Kabul. Wiki iliyopita, timu yetu ilienda kwenye kambi ya wakimbizi wa ndani na kuona kazi kubwa inayofanywa huko na timu za wahudumu wa afya wa UNICEF, ingawa kama ilivyoelezwa na shirika la Umoja wa Mataifa la afya WHO, shughuli zimesimama katika siku chache zilizopita na tunatarajia kuanza tena operesheni hivi karibuni. Kuna uhitaji mkubwa lazima tuendelee kusaidia."

Nalo shirika la Umoja wa Mataifa la uhamiaji IOM limekuwa likifuatilia kwa wasiwasi mkubwa maendeleo nchini Afghanistan na matokeo mabaya kwa watu waliohamishwa na vita makwao pamoja na raia wanaohitaji msaada wa kibinadamu, katika nchi ambayo tayari imeathiriwa sana na miaka mingi ya mizozo na ukame.  

Kupitia taarifa yake iliyotolewa leo IOM imesema  “Kwa sababu ya kutokuwa na utulivu na maendeleo ya hivi karibuni ya usalama katika mji mkuu Kabul, harakati za kwenda na kutoka nchini humo zimezuiliwa, na kuathiri shughuli za IOM za misaada. Kwa kuzingatia ukosefu wa usalama uliopo kote nchini, zoezi la kurejea iiari kwa usaidizi wa shirika hilo pamoja na shughuli zake za kuwajumuisha katika jamii wanaowasili kwa sasa zimesitishwa kwa muda.."


TAGS: OHCHR, UNICEF, IOM, Afghanistan, Taliban, machafuko, misaada, haki za binadamu