Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Sasa ni wakati wa kuepusha vita isiyo na ukomo Afghanistan – Guterres

Mama na mwanae katika kambi ya Haji ambayo inahifadhi wakimbizi wa ndani huko Kandahar, Afghanistan
© UNICEF Afghanistan
Mama na mwanae katika kambi ya Haji ambayo inahifadhi wakimbizi wa ndani huko Kandahar, Afghanistan

Sasa ni wakati wa kuepusha vita isiyo na ukomo Afghanistan – Guterres

Amani na Usalama

Huu ni wakati wa Afghanistan kuacha mashambulizi, huu ni wakati wa kuanza mazungumzo makini na huu ni wakati wa kuepusha vita vya wenyewe kwa wenyewe visivyokoma, ndivyo ambavyo Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterres ametamatisha mkutano wake na waandishi wa habari hi leo jijini New York, Marekani baada ya kurejea tu kutoka likizo.

Ametoa kauli hiyo wakati inaelezwa kuwa hali ya usalama na kibinadamu inazidi kuzorota nchini Afghanistan mapigano yakiripotiwa katika majimbo 33 kati ya 34 ya taifa hilo la barani Asia.

Katibu Mkuu amesema mapigano kati ya watalibani na vikosi vya usalama vya serikali kwenye maeneo ya mijini yanasababisha machungu makubwa, idadi ya wakimbizi wa ndani inaongezeka, halikadhalika vifo na majeruhi na zaidi ya yote, “hospitali zimefurika, vifaa vya matibabu na vyakula vinapungua. Barabara, shule, kliniki na miundombinu mingine muhimu imeharibiwa.”

Amesema kila uchao, mzozo huo unakuwa na madhara makubwa zaidi kwa wanawake na watoto hivyo, “natoa wito kwa pande zote ziitikie wito juu ya madhara makubwa ya mapigano kwa raia na kwamba wanapaswa kulinda raia. Watekelezaji wafikishwe mbele ya sheria ili wawajibishwe.”

Raia kwenye maeneo ya watalibani wanateseka

Katibu Mkuu amesema anachukizwa pia na viashiria vya awali ya kwamba watalibani wameweka vikwazo vikali dhidi ya haki za kibinadamu kwenye maeneo yaliyo chini ya udhibiti wao wakilenga zaidi wanawake na waandishi wa habari.

Mtoto wa miaka mitano, akiwa amembeba mdogo wake wakiume wakiwa kambi ya watu waliokimbia makazi yao huko Kandahar, kusini mwa Afghanistan.
© UNICEF Afghanistan
Mtoto wa miaka mitano, akiwa amembeba mdogo wake wakiume wakiwa kambi ya watu waliokimbia makazi yao huko Kandahar, kusini mwa Afghanistan.

“Inatisha sana na kuvunja moyo kuona taarifa ya kwamba haki za kibinadamu kwa wanawake na wasichana nchini Afghanistan ambazo zilitambuliwa kwa ugumu sasa zinasambaratishwa,” amesema Katibu Mkuu.

Amesema ujumbe kutoka jamii ya kimataifa kwenda kwa wale walio kwenye mapigano ni dhahiri kwamba, “kushika madaraka kwa njia ya kijeshi ni mbinu isiyo sahihi. Hiyo inaweza tu kuongeza vita vya wenyewe kwa wenyewe au kutengwa kabisa kwa Afghanistan.”

“Hospitali zimefurika, vifaa vya matibabu na vyakula vinapungua. Barabara, shule, kliniki na miundombinu mingine muhimu imeharibiwa" - António Guterres, Katibu Mkuu UN

Ametoa wito kwa wataliban kukomesha mapigano na kushauriana na pande nyingine kwa nia njema na kwa maslahi ya wananchi wa Afghanistan.

Bwana Guterres amesema ni matumaini yake kuwa mashauriano huko Doha, Qatar kati ya wawakilishi wa serikali ya Afghanistan na watalibani ambayo yanaungwa mkono na jamii ya kimataifa, yataweza kurejesha njia sahihi ya suluhu ya kudumu nchini humo.

Guterres amekumbusha kuwa ni suluhu ya kisiasa pekee inayoongozwa na waafghanistan ndio inaweza kutoa hakikisho la amani na kwamba Umoja wa Mataifa kwa upande wake umeazimia kuchangia katika suluhu hiyo, na kusongesha haki za wananchi wa Afghanistan sambamba na kutoa misaada ya kibinadamu inayozidi kuongezeka miongoni mwa raia wenye uhitaji ambao nao idadi yao inaongezeka.