Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

12 wauawa katika shambulio Afghanistan, Guterres atuma rambirambi

Picha UNAMA / Fardin Waezi
Kabul, katikati ya maisha ya kisiasa na kijamii ya Afghanistan.

12 wauawa katika shambulio Afghanistan, Guterres atuma rambirambi

Amani na Usalama

Msikiti unaotumika pia kusajili wapiga kura nchini Afghanistan washambuliwa.

Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterres amelaani vikali shambulio la leo huko Afghanistan ambapo yaripotiwa watu 12 wameuawa na makumi kadhaa wamejeruhiwa.

Yaelezwa kuwa mlipuko umetokea katika msikiti mmoja kwenye jimbo la Khost, wakati watu wakiwa wamekusanyika kwa sala ya mchana. Msikiti huo pia ni kituo cha kujiandikishia wapiga kura.

Kupitia msemaji wake, Bwana Guterres ametuma salamu za rambirambi kwa familia za wafiwa huku akiwatakia ahueni ya haraka majeruhi.

Halikadhalika Katibu Mkuu ameonyesha mshikamano wake na wananchi wa Afghanistan ambao amesema wanasaka kutekeleza haki yao ya msingi ya kikatiba kwa kujiandika ili kushiriki uchaguzi ujao wa wabunge.

Tarehe 22 mwezi uliopita mshambuliaji mmoja alijilipua karibu na kituo cha kujiandikishia wapiga kura kwenye mji mkuu Kabul ambako watu 57 waliuawa.

Uchaguzi huo wa wabunge utafanyika nchini Afghanistan mwezi Oktoba mwaka huu.