Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

UNHCR yapata uwezo wa kufikia wakimbizi Tigray

UNHCR na serikali ya EEthiopia ikiandikisha wakimbizi kutoka Eritrea Addis Ababa,
© UNHCR/Olga Sarrado Mur
UNHCR na serikali ya EEthiopia ikiandikisha wakimbizi kutoka Eritrea Addis Ababa,

UNHCR yapata uwezo wa kufikia wakimbizi Tigray

Wahamiaji na Wakimbizi

Hatimaye shirika la Umoja wa Mataifa la kuhudumia wakimbizi, UNHCR na wadau wake wamepata tena uwezo wa kuingia katika kambi za wakimbizi za Mai Aini na  Adi Harush zinazohifadhi wakimbii wa Eritrea nchini Ethiopia. Hatua ya sasa inakuja baada ya kushindwa kuingia kambini huko tangu tarehe 13  mwezi uliopita wa Julai kutokana na mapigano jimboni humo. 

Msemaji wa UNHCR mjini Geneva Uswisi Boris Cheshirkov amewaeleza waandishi wa habari hii leo kuwa usambazaji wa misaada kwenye kambi zote ulianza tarehe 5 mwezi huu wa Agosti kwa wakimbizi wote 23,000. 

Hata hivyo hali tete ya usalama na vikwazo vya kuingia bado vinasababisha wakimbizi waishi kwenye mazingira magumu. 

Huduma za msingi kama vile afya hazipo huku maji safi ya kunywa yanakaribia kuisha. 

“UNHCR inatoa wito wa kuwepo kwa njia salama ya kupita itakayoruhusu wakimbizi kuondoka kambini Mai Aini na Adi Harush na kuhamishiwa eneo jipya la Alemwach, karibu na mji wa Dabat ulioko umbali wa takribani kilomita 135. 

UNHCR inasisitiza kuwa pande zote kwenye mzozo zitoe hakikisho la kuingiia jimboni Tigray na kwingineko bila vikwazo vyovyote  ili shirika hilo na wadau waweze kusambaza misaada muhimu na kulinda makumi ya maelfu ya wanaohitaji misaada ya dharura.