Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Dola milioni 156 zahitajika kusaidia wanaokimbia ghasia Tigray- UNHCR

Mkimbizi kutoka Tigray akisubiri mgao wa chakula makazi ya Um Rakuba nchini Sudan.
WFP/Arete/Joost Bastmeijer
Mkimbizi kutoka Tigray akisubiri mgao wa chakula makazi ya Um Rakuba nchini Sudan.

Dola milioni 156 zahitajika kusaidia wanaokimbia ghasia Tigray- UNHCR

Wahamiaji na Wakimbizi

Shirika la Umoja wa Mataifa la kuhudumia wakimbizi, UNHCR pamoja na wadau 30 wa kibinadamu  hii leo wanatoa wito wa dharura kupatiwa wa dola milioni 156.
 

Fedha hizo zinahitajika ili kupatia mahitaji muhimu ya kibinadamu kwa wakimbizi wa Ethiopia wanaokimbia mzozo katika jimbo la Tigray, na zitatumika katika miezi minne ya kwanza ya mwaka 2021.
 
Msemaji wa UNHCR Babar Baloch akizungumza na waandishi wa habari hii leo huko Geneva, Uswisi amesema fedha hizo zitasaidia katika maandalizi ya kuwapokea wakimbizi kwenye nchi zingine za eneo hilo iwapo watu zaidi watahama.
 
Katika kipindi cha majuma sita yaliyopita zaidi ya wakimbizi 52,000 kutoka  eneo la Tigray  wamekimbilia Sudan.
 
Licha kuwa idadi ya wakimbizi wanaowasili inapungua siku za hivi karibuni hadi wakimbizi 500 kwa siku, mashirika ya kutoa misaada yanakumbana na huduma za dharura katika eneo ambalo halijawai kushuhudia kiwango kikubwa cha wakimbizi kwa miongo kadhaa.
 
Mpango wa maandalilzi ya kuwapokea wakimbizi kutokana na mzozo wa Tigray ni wa kipindi cha kuanzia Novemba 2020 hadi Juni 2021 na unalenga hadi wakimbizi 115,000 na jamii 22,000 zinazowapa hifadhi.
 
Bwana Baloch amesema unalenga kusaidia serikali za Sudan, Djibouti na Eritrea kutoa huduma za kuokoa maisha kwa wale ambao wamelazimika kukimbia makwao.
 
Kati ya huduma ambazo zitapewa kipaumbele ni pamoja ni utoaji chakula, huduma za afya na elimu na kusaidia makundi yaliyo na mahitaji maalumu kama vile wanawake na wasichana walio kwenye hatari.
 
Mashariki mwa Sudan kuanzia Novemba 14 hadi sasa zaidi ya wakimbizi 20,000 wamehamishwa kutoka maeneo ya mpakani kwenda kambi ya Um Rakuba iliyo umbali wa kilomita 75 kutoka mji wa Gedaref.
 
Kwa sasa wakimbizi wengi wamesalia  maeneo yenye misongamano na mazingira dunia ambapo pia kunashuhudiwa uhaba ya madawa na huduma zingine.
 
Hadi sasa ni asilimia 30 ya dola milioni 46 ya fedha zinazohitajika zimepokewa na UNHCR na pia washirika katika mpango huu.