Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Chukueni hatua haraka, hali Afghanistan ‘si hali’- Lyons

Watu waliokimbia makazi yao nchini Afghanistan kutokana na ukosefu wa usalama wakiwa kwenye kambi ya wakimbizi wa ndani huko Herat.
IOM/Muse Mohammed
Watu waliokimbia makazi yao nchini Afghanistan kutokana na ukosefu wa usalama wakiwa kwenye kambi ya wakimbizi wa ndani huko Herat.

Chukueni hatua haraka, hali Afghanistan ‘si hali’- Lyons

Amani na Usalama

Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa limeombwa lichukue hatua za haraka hivi sasa ili kuepusha hali mbaya zaidi ya usalama nchini Afghanistan wakati huu ambapo vita nchini humo imekuwa mbaya na ya uharibifu zaidi.

 

Wito huo umetolewa leo na Mwakilishi Maalum wa Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa nchini Afghanistan Bi. Deborah Lyons wakati akihutubia kikao cha Baraza la Usalama kilichokutana kujadili hali ya usalama katika taifa hilo la Asia ambako usalama unadorora kila uchao.

Bi. Lyons ambaye pia ni Mkuu wa ujumbe wa Umoja wa Mataifa nchini Afghanistan, UNAMA, amesema “kitengo cha watalibani kuendelea kusonga mbele katika miezi ya hivi karibuni na kukaribia miji mikubwa kinatukumbusha vita vya Syria na vile vya Balkan.”

Amesema Afghanistan hivi sasa iko katika nyakati ya kipekee mbele ikiwa inakabiliwa na mashauriano ya dhati ya amani au majanga yaliyochangamana ambayo ni mzozo mbaya na hali mbaya ya kibinadamu ikifungamana na ukiukwaji wa haki za binadamu.”

Akionya kwamba madhara ya hali ya sasa yanaweza kuvuka mipaka ya Afghanistan, Bi. Lyons amesihi wajumbe wa Baraza la Usalama kutumia fursa ya sasa na kuonesha azma yao ya “kuzuia Afghanistan isitumbukie kwenye janga ambalo pengine halijawahi kushuhudiwa katika karne ya sasa.”

Deborah Lyons, Mwakilishi Maalum wa Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa nchini Afghanistan akihutubia Baraza la Usalama kuhusu hali ya Afghanistan
UN Photo/Loey Felipe
Deborah Lyons, Mwakilishi Maalum wa Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa nchini Afghanistan akihutubia Baraza la Usalama kuhusu hali ya Afghanistan

Aina tofauti ya vita 

Baada ya kuteka maeneo ya vijijini kufuatia kuondoka kwa majeshi ya kimataifa, watalibani hivi sasa wanasongea miji mikubwa na miji mikuu ya majimbo ya Kandahar, Herat na Lashkar Gah.
Idadi ya watu waliopoteza maisha kutokana na mashambulizi ya wataliban ni zaidi ya 1,000 katika maeneo hayo matatu kwa mwezi uliopita pekee, ambako nyumba, hospitali, madaraja na miundombinu mingine imeharibiwa.

Mapigano makali  yameripotiwa Laskhar Gah, mji mkuu wa jimbo la Helmand kusini mwa Afghanistan ambako takribani watu 104 ambao ni raia waliuawa na 403 walijeruhiwa katika kipindi cha siku 10 pekee.

“Hii ni aina nyingine ya vita, ikitukumbusha vita ya hivi karibuni Syria n akule Sarajevo. Kushambulia maeneo ya mijini ni kwa sababu ya makusudi ili kuleta madhara makubwa kwa raia,” amesema Mkuu huyo wa UNAMA.

Mamluki wanapata msaada

Kwa mujibu wa Mwakilishi wa kudumu wa Afghanistan kwenye Umoja wa Mataifa balozi Ghulam M. Isaczai, watalibani hawapambani peke yao bali wanapata msaada akisema, “zaidi ya wapiganaji mamluki 10,000 wako nchini mwetu wakiwakilisha zaidi ya vikundi 20 vikiwemo vile vya Al Qaeda na ISIL.”

Amesema kuna ushahidi tosha kuwa kikundi cha East Turkestan Islamic Movement na the Islamic Movement of Uzbekistan, ambavyo vimekiri uaminifu wao kwa ISIL, vinapambana upande wa wataliban kwenye majimbo ya Faryab, Jowzjan, Takhar na Badakhshan ambako hivi sasa wako na familia zao chini ya udhibiti wa wataliban.

Balozi Isaczai akihutubia kwa niaba ya Waziri wa Mambo ya Nje wa Afghanistan, amesema ushirikiano wa sasa kati ya wataliban na vikundi hivyo vya kigeni vya kigaidi ni mkubwa kuliko wakati wowote ule.

Tumeni ujumbe thabiti

Kuelekea mkutano wa wiki ijayo huko Qatar na mkutano ujao wa Baraza la Usalama mwezi ujao kuhusu Afghanistan, Bi. Lyons ameomba wajumbe wa Baraza watumie fursa ya sasa kusaka suluhu ya kudorora kwa usalama Afghanistan.

Amesema Baraza la Usalama lazima litoe taarifa isiyo na utata dhidi ya mashambulizi ya miji ya kwamba yakome, na kwamba nchi zitakapokutana na wawakilishi wa watalibani wawajulishe kuwa ni lazima wasitishe mapigano na mazungumzo yarejee.