Tunalaani vikali shambulio la Kabul Afghanstan - UNICEF 

8 Mei 2021

Shirika la Umoja la Umoja wa Mataifa la kuhudumia watoto, UNICEF limelaani vikali shambulio lililotokea mapema leo Jumamosi, karibu na shule ya sekondari ya "Syed Al-Shuhada" huko Kabul, Afghanistan. 

Shambulio hilo la mlipuko limeua watoto wanafunzi, wengi wao wakiwa wasichana, na kusababisha majeraha mengi makubwa. 

Katika taarifa iliyotolewa na UNICEF mjini New York, Marekani, Mkurugenzi Mtendaji wa UNICEF, Henrietta Fore amesema kuwa vurugu katika shule au karibu na shule hazikubaliki kabisa. "Shule zinapaswa kuwa mahali pa amani ambapo watoto wanaweza kucheza, kujifunza na kujumuika salama," na shirika hilo limetaka watoto wasiwe walengwa wa vurugu. 

UNICEF imerejelea kuwa inaendelea kutoa wito kwa pande zote kwenye mzozo huo kutii sheria za kimataifa za haki za binadamu na sheria za kimataifa za kibinadamu na kuhakikisha usalama na ulinzi wa watoto wote. 

Kupitia mtandao wa tweeter, Rais wa Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa, Volkan Bozkir, ameuelezea mlipuko huo karibu na shule mjini Kabul kama shambulio la chuki na la woga. 

"Nimesikitishwa sana na maisha ya watu yaliyopotea na majeruhi kadhaa, hasa wanafunzi wadogo. Ninalaani kulengwa kwa raia wasio na hatia na ninatuma salamu zangu za rambirambi kwa serikali na watu wa Afghanistan." Ametuma ujumbe Bwana Bozkir. 

Kwa upande wa Ujumbe wa Umoja wa Mataifa nchini Afghanistan, UNAMA, bomu hilo ni "unyama". Ujumbe huo umetuma ujumbe wake wa masikitiko na kutuma ujumbe wa pole kwa familia za waathirika, ukiwatakia kupona haraka wale waliojeruhiwa katika shambulio hilo. 

Shule ya sekondari ya Sayed Ul-Shuhada iko katika kitongoji cha Dasht-e-Barchi magharibi mwa Kabul, makazi ya wengi kutoka kundi la watu wa chache wa jamii ya Hazari ambao zaidi ni waumini wa Shia.  Kufikia sasa hakuna kundi ambalo limedai kuhusika na shambulio hilo, lakini eneo hilo limekuwa likilengwa mara kwa mara na wanamgambo wa Kiislam wa Kisuni. 

  

 

  

 

♦ Iwapo ungependa kupokea taarifa kutoka UN News Kiswahili kila wakati zinapochapishwa jisajili  hapa.
♦ Pia unaweza kupakua apu ili kusikiliza matangazo yetu wakati wowote popote ulipo.
♦ Tembelea pia chaneli yetu ya Youtube na pia Soundcloud na Twitter