Shambulio uwanjani Kabul laua watu kadhaa na wengine wengi wajeruhiwa, UN yalaani

Muonekano wa mji wa Kabul, Afghanistan
Photo UNAMA/Fardin Waezi
Muonekano wa mji wa Kabul, Afghanistan

Shambulio uwanjani Kabul laua watu kadhaa na wengine wengi wajeruhiwa, UN yalaani

Amani na Usalama

Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterres amelaani shambulio la leo huko nchini Afghanistan ambalo limesababisha vifo vya raia kadhaa na wengine wamejeruhiwa.

Taarifa iliyotolewa leo jijini New York, Marekani na Naibu Msemaji wa Umoja wa Mataifa Farhan Haq imesema shambulio hilo limetokea katika uwanja kimataifa wa mchezo wa kriketi kwenye mji mkuu wa Afghanistan, Kabul.

Katibu Mkuu ametuma salamu za rambirambi kwa familia za waliopoteza maisha na kutakia ahueni ya haraka majeruhi.

Amesisitiza kuwa mashambulizi dhidi ya rai ana maeneo ya raia ni kinyume cha sheria za kimataifa za kibinadamu.

Kwa mujibu wa vyombo vya habari, mlipuko ulitokea wakati mchezo ukiendelea katika siku hii ya Ijumaa ambayo huwa ni siku ya mapumziko Afghanistani.

Naye Naibu Mwakilishi wa Katibu Mkuu wa  Umoja wa Mataifa nchini Afghanistan Dkt. Ramiz Alakbarov ambaye alikuwa uwanjani akishuhudia mechi hiyo, amelaani shambulio hilo akisema ni la kikatili.
Dkt. Alakbarov ambaye pia ni Naibu Mkuu wa ujumbe wa Umoa wa Mataifa nchini Afghanistan, UNAMA alikwepo uwanjani hapo pia kuhutubia chama cha Kitaifa cha kriketi nchini humo na ametuma salamu za rambirambi kwa wafiwa na kutakia ahueni ya haraka majeruhi.

Taarifa iliyotolewa na UNAMA mjini Kabul, imemnukuu akitaka uchunguzi ufanyike na wahusika wafikishwe mbele ya sheria.