Hospitali ya wazazi yashambuliwa Kabul, miongoni mwa waliouawa ni watoto wachanga

12 Mei 2020

Katika shambulio la kwanza kwenye hospitlai ya wazazi katika mji mkuu, Kabul, watu 14 wakiwemo watoto wawili wachanga waliuawa  baada ya watu wenye silaha kushambulia hospitali ya wazazi ya Sad Bistar.
 

Shambulio lingine limetokea baada ya mtu mmoja kujilipua na kuua watu wapatao 24 na kujeruhi wengine wengi wakati wa mazishi mjini Nangahar, mashariki mwa Afghanistan.

Ujumbe wa Umoja wa Mataifa nchini Afghanistan, UNAMA kupitia mtandao wake wa Twitter, umeelezea kushtushwa na matukio hayo.

UNAMA imetaka mamlaka nchini Afghanistan isake wahusika na wafikishwe mbele ya sheria huku ikituma salamu za rambirambi kwa familia za wafiwa.

Mratibu wa masuala ya kibinadamu wa Umoja wa Mataifa nchini Afghanistan, Toby Lanzer amesema amechukizwa na shambulio hilo kwenye hosptali ya wazazi ya Sad Bistar, ambayo wakati huo ilikuwa imejaa wagonjwa na wafanyakazi.

Katika taarifa yake, amesema kuwa ni jambo la kutoamini ya kwamba shambulio hilo limefanywa wakati Afghanistan inana kukabiliana na janga la ugonjwa wa virusi vya Corona, au COVID-19.

Amekumbusha kuwa raia waliokuwa wakipata huduma kwenye hospitali hiyo yenye vitanda 100, pamoja na wahudumu wa afya, miundombinu ya tiba na wafanyakazi wa kujitolea wote wanalindwa na sheria ya kimataifa ya kibinadau na kwamba ukiukwaji wake lazima uchunguwe na wahusika wafikishwe mbele ya sheria.
 

 

♦ Tafadhali iwapo unataka kupokea taarifa kutoka UN News Kiswahili kila wakati zinapochapishwa jisajili  hapa.
♦ Pia unaweza kupakua apu ili kusikiliza matangazo yetu wakati wowote popote ulipo.
♦ Tembelea pia chaneli yetu ya Youtube na pia Soundcloud