Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Watoto wetu wanahitaji chakula. Wanaweza kutaka chochote, hawajui kama tunacho au la - Afghanistan  

Nchini Afghanistan, licha ya kuwa eneo zuri kwa kilimo watu wengi awapati mazao ya kutosha
UNAMA/Eric Kanalstein
Nchini Afghanistan, licha ya kuwa eneo zuri kwa kilimo watu wengi awapati mazao ya kutosha

Watoto wetu wanahitaji chakula. Wanaweza kutaka chochote, hawajui kama tunacho au la - Afghanistan  

Msaada wa Kibinadamu

Shirika la Umoja wa Mataifa la kuhudumia wakimbizi UNHCR na wadau wake wanawasaidia raia wa Afghanstan waliokimbia makazi yao kwa kuwapatia makazi ya dharura, chakula, huduma ya afya, msaada wa maji, huduma za kujisafi na msaada wa pesa, lakini uhaba wa ufadhili unamaanisha rasilimali za misaada ya kibinadamu zinapungua sana.

Mama mjane wa watoto wanne anayejitahidi kutunza familia yake ni miongoni mwa Waafghani 330,000 waliofurushwa katika makazi yao tangu kuanza kwa mwaka huu kutokana na kuongezeka kwa mapigano. Mama huyu anasema, "kulikuwa na vita. Mabomu yalikuwa yakirushwa. Baba yangu aliuawa huko, na jamaa zangu wengi waliuawa pia, na ilibidi tukimbie. Niliwajibika kwa watoto wangu na sikutaka wauawe. Kwa hivyo, nilikuja hapa na mama yangu mzee.” 

Maryam [sio jina lake halisi] na familia yake wamejazana katika kivuli cha makazi ya muda katika kambi nje kidogo ya mji wa Mazar-e Sharif kaskazini mwa Afghanistan wakitafuta pumziko kutokana na joto la nyuzijoto 45 za Selsiasi nje. Ingawa mahema ya plastiki yapo, joto kali linawafanya wasiweze kuyatumia, kwa hivyo wakazi wa kambi hutegemea vitu kama mashuka kujikinga na jua kali na dhoruba za vumbi za mara kwa mara. Maryam anasema, "hali yetu ni ngumu sana. Kama unavyoona, sisi sote tumehama. Watoto wetu wanahitaji chakula. Wanaweza kutaka chochote, wao ni watoto, hawajui kama tunacho au la. " 

Mzozo unapozidi kaskazini mwa Afghanistan na maeneo mengine ya nchi, UNHCR, inaonya ikisema kutofikia makubaliano ya amani kutasababisha kufurushwa zaidi kwa watu. 

Fahim Hamdard, ni Ofisa wa UNHCR katika eneo hilo anasema,  "Katika mwaka jana, familia zimekuwa zikishughulikia janga la COVID-19, ukame mbaya na sasa kuongezeka kwa vurugu katika maeneo ya kaskazini na kaskazini mashariki inawasukuma watu zaidi kutoka nyumba zao kila siku." 

Katikati ya ongezeko la jumla la vifo vya raia, idadi ya wanawake na watoto walioathiriwa na vurugu imeongezeka sana tangu mwezi Januari, na juu ya  mzozo wa miongo kadhaa wa Afghanistan vimewaathiri watu kama Maryam na familia yake.