Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Ziara yetu Tigray imethibitisha hali tete inayokabili watoto- UNICEF

Mtoto akipimwa utapiamlo katika kituo cha afya jimboni Tigray nchini Ethiopia
© UNICEF/Mulugeta Ayene
Mtoto akipimwa utapiamlo katika kituo cha afya jimboni Tigray nchini Ethiopia

Ziara yetu Tigray imethibitisha hali tete inayokabili watoto- UNICEF

Msaada wa Kibinadamu

Hali tete iliyokuwa inadhaniwa kukumba watoto jimboni Tigray nchini Ethiopia sasa imethibitishwa baada ya watendaji wa shirika la Umoja wa Mataifa la kuhudumia watoto, UNICEF kuweza kufika eneo hilo baada ya kushindwa kufanya hivyo kwa miezi kadha kutokana na ukosefu wa usalama.
 

UNICEF inakadiria kuwa zaidi ya watoto 10,000 jimboni Tigray wanaweza kukumbwa na utapiamlo uliokithiri katika kipindi cha miezi 12 ijayo ikiwa ni ongezeko la mara 10 ikilinganishwa na mwaka mzima,” amesema Marixie Mercado, msemaji waUNICEF huko mjini Geneva Uswisi.

Akizungumza na waandishi wa habari hii leo, Bi. Mercado amesema “takwimu za uchunguzi wa afya ya wanawake zinaonesha kuwa takribani nusu ya wanawake wajawazito na wanaonyonyesha sawa na asilimia 47  wana utapiamlo uliokithiri. Viwango hivi vya kusikitisha vinadokeza kuwa akina mama wanaweza kukabiliwa na matatizo yanayohusiana na ujauzito na hivyo kuongeza hatari ya kufariki dunia wakati wa kujifungua sambamba na watoto kuzaliwa na uzito mdogo na hivyo kuweza kupata magonjwa au kufariki dunia.”

Takwimu hizo anazozungumzia zinafuatia uchunguzi wa wajawazito uliofanywa na UNICEF na wadau tangu kulipuka kwa mzozo huko Tigray mwezi Novemba mwaka jana.

Bi. Mercado amesmema janga la utapiamlo linakumba eneo ambalo kuna uharibifu wa mifumo ya chakula, afya, lishe, maji na huduma za kujisafi ambayo watoto na familia zao wanaitegemea ili waweze kuishi.

Mama ambaye amefurushwa kutoka ukanda wa Magharibi wa Tigray nchini Ethipia akizungumza na mfanyakazi wa UNICEF mjini Mekelle
UNICEF/Esiey Leul Kinfu
Mama ambaye amefurushwa kutoka ukanda wa Magharibi wa Tigray nchini Ethipia akizungumza na mfanyakazi wa UNICEF mjini Mekelle

Mathalani katika maeneo ya Wajirat na Gijet, wilaya mbili ambazo hazikuweza kufikiwa tangu kuanza kwa mzozo Tigray, “kile nilichoona ni mchanganyiko wa mazingira ambayo yanaweka maisha ya watoto hatarini:katika maeneo mengi hakukuwepo na misaada ya vyakula vya kuwaongezea nguvu ambavyo vinahitajika ili kutibu utapiamlo uliokithiri. Hakuna dawa za viuvijasumu au antibayotiki. Vituo vya afya havina umeme, na zaidi ya yote, watoto hawajapatiwa chanjo kwa miezi kadhaa,” amesema Msemaji huyo wa UNICEF akirejelea ziara yake kwenye maeneo hayo.

Hata hivyo amesema kurejea huduma za lishe, afya na chakula kunahitaji msaada wa kibinadamu uongezwe kwa kiasi kikubwa.

“Hii ina maana kwamba watoa misaada lazima waruhusiwe kufanya kazi zao bila vikwazo, mathalani waweze kupata mafuta, fedha, mawasiliano ili wafikishe misaada. Bila kufanya hivyo basi misaada itakwama.”

Hata hivyo amesema pamoja na yote, UNICEF na wadau wanatoa wito kwa pande kinzani kuheshimu wajibu wao wa kimataifa wa kulinda watoto dhidi ya hatari.