Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Watoto zaidi ya milioni 2 hawajafikiwa na msaada Tigray machafuko yakiendelea:UNICEF 

Wakimbizi waliowasili kutoka Tigray Ethiopia wakileta msaada kwa ajili ya kukarabati makazi kambi ya Raquba, Kassal, Sudan.
UNFPA/Sufian Abdul-Mouty
Wakimbizi waliowasili kutoka Tigray Ethiopia wakileta msaada kwa ajili ya kukarabati makazi kambi ya Raquba, Kassal, Sudan.

Watoto zaidi ya milioni 2 hawajafikiwa na msaada Tigray machafuko yakiendelea:UNICEF 

Wahamiaji na Wakimbizi

Watoto wapatao milioni 2.3 kwenye jimbo la Tigay nchini Ethiopia bado hawajafikiwa na msaada wa kibinadamu huku machafuko yaliyoanza mwezi Novemba mwaka huu yakiendelea limesema shirika la Umoja wa Mataifa la kuhudumia watoto UNICEF. 

Katika ujumbe uliotolewa leo mjini New York Marekani mkurugenzi mtendaji wa shirika hilo Henrietta Fore amesema “Tunatyiwa hofu kubwa kwamba kuendelea kucheleweshwa zaidi kwa fursa ya kuwafikia Watoto hao ndivyo hali inavyozidi kuwa mbaya kwani msaada wa chakula kikiwemo ambacho kimeshatayarishwa kwa ajili ya kutibu Watoto utapiamlo, madawa, maji, mafuta na msaada mwingine wa muhimu umeenza kupungua. Kuwalinda Watoto hawa ambao wengi ni wakimbizi na wakimbizi wa ndfani, na kuwapa msaada wa kibinadamu inapaswa kuwa kipaumbele.” 

Bi. Fore amesisitiza kuwa UNICEF na washirika wake wa misaada ya kibinadamu wako tayari kutoa msaada wa kuokoa maisha ikiwemo matibabu kwa watoto wenye utapiamlo, madawa, maji na bidhaa zingine za msingi.  

Hadi sasa amesema UNICEF imeshatoa baadhi ya msaada kwa washirika wao walioko Tigray lakini msaada huo hautoshi. 

“Tunahitaji kutoa msaada unaoendana na mahitaji Tigray na tunahitaji kupata fursa kamili ya kuweza kutathimini ukubwa wa mahitaji ya Watoto jimboni humo. Hivyo tunatoa wito wa kupewa fursa ya kufikisha misaada ya kibinadamu ambayo ni ya haraka, endelevu, isiyo na mashariti ili tuzifikie familia zenye mahitaji popote zilizpo.” 

UNICEF pia imeitaka serikali ya Ethiopia kuruhusu raia wanaotaka kuondoka kwenda kusaka usalama wafanye hivyo pengine nah ii inajumuisha wale wanaotaka kuvuka mpaka na kusaka ulinzi wa kimataifa. 

Shirika hilo limesisitiza kwamba “Kukidhi mahitaji muhimu ya msingi ya Watoto na wanawake hakupaswi kuchelewesha hata kidogo.”