Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Maisha ya watu milioni 20 yako njiapanda Ethiopia kutokana na vita, ukame na uhaba wa chakula:WFP

Familia iliyofurushwa makwao huko Tigray nchini Ethiopia ikiwa katika makazi ya muda huko wilaya ya Asgede, Tigray na wamepatiwa msaada wa chakula na WFP
WFP/Claire Nevill
Familia iliyofurushwa makwao huko Tigray nchini Ethiopia ikiwa katika makazi ya muda huko wilaya ya Asgede, Tigray na wamepatiwa msaada wa chakula na WFP

Maisha ya watu milioni 20 yako njiapanda Ethiopia kutokana na vita, ukame na uhaba wa chakula:WFP

Msaada wa Kibinadamu

Njaa inazidi kuwazonga zaidi ya waethiopia milioni 20 ambao wanakabiliwa na vita kaskazini mwa nchi hiyo, ukame katika eneo la kusini na kupungua kwa msaada wa chakula na lishe kuanzia mwezi ujao, limeonya shirika la Umoja wa Mataifa la mpango wa chakula duniani WFP 

Katika onyo hilo lililotolewa leo kupitia taarifa yake WFP inasema "Mchanganyiko wa migogoro na ukame umesababisha ongezeko la mfumuko wa bei na hadi mwezi Aprili mwaka huu mwelekeo wa bei ya chakula nchini Ethiopia ulipanda kwa asilimia 43 ikilinganishwa na mwezi kama huo mwaka jana. Wakati huo huo, bei za mafuta ya mboga na nafaka zimemekuwa zikipanda kwa zaidi ya asilimia 89 na asilimia 37 mwaka hadi mwaka.” 

Vita na njaa 

Kwa mujibu wa WFP, miezi 19 ya vita imewaacha zaidi ya watu milioni 13 kaskazini mwa taifa hilo la Pembe ya Afrika wakihitaji msaada wa wa kibinadamu wa chakula, hasa katika maeneo yaliyoathiriwa na migogoro katika majimbo ya Afar, Amhara na Tigray. 

Katika kipindi cha miezi miwili iliyopita, tangu serikali itangaze usitishaji wa uhasama kwa ajili ya misaada ya kibinadamu misaada ya, chakula na vifaa vya kibinadamu vimekuwa vikimiminika katika eneo la Tigray. 

Na wakati WFP imewasilisha zaidi ya tani 100,000 za chakula tangu Aprili Mosi zinazotosha kulisha watu milioni 5.9 kwa mwezi  usambazaji wa mafuta haujashika kasi. 

Chini ya nusu ya lita milioni mbili za mafuta zinazohitajika zimeingia katika eneo hilo katika wiki za hivi karibuni. 

Hatimaye WFP imeweza kukidhi mahitaji ya chakula ya zaidi ya watu 800,000 huko Tigray na imekamilisha hivi karibuni kusambaza mgao wa dharura wa chakula kwa watu milioni 1.3 huko Afar na Amhara. 

Mkimbizi wa ndani akiwa amebeba mwanae huko Mekelle, mji mkuu wa jimbo la Tigray nchini Ethiopia.
©UNICEF/ Esiey Leul
Mkimbizi wa ndani akiwa amebeba mwanae huko Mekelle, mji mkuu wa jimbo la Tigray nchini Ethiopia.

Hatari za kiafya 

Huko Tigray, zaidi ya asilimia 20 ya watoto wenye umri wa chini ya miaka mitano, na nusu ya wanawake wajawazito na wanaonyonyesha, wana utapiamlo, kwa mujibu wa WFP. 

Wakati huo huo, asilimia 32 ya wazazi katika ukanda wa 4 wa Afar, mojawapo ya kanda tano za utawala katika eneo hilo na asilimia 16 huko Amhara kumeripotiwa kuwa katika kipindi cha miezi mitatu iliyopita, utapiamlo ulisababisha watoto wao wa chini ya miaka mitano kupelekwa kwenye kituo cha afya. 

Tathmini ya hivi laribuni ya WFP ya maeneo yaliyoathiriwa na migogoro katika majimbo yote mawili yamelitaja tatizo hili pia. 

Na katika maeneo ya kusini na kusini-mashariki mwa Ethiopia, wastani wa watu milioni 7.4 huamka na njaa kila siku wakati nchi ikikabiliana na msimu wa nne mfululizo wa kutokuwa na mvua mfululizo. 

Vita ya Ukraine yachochea mgogoro wa chakula 

 

WFP inasema wakati huo huo, athari mbaya za vita nchini Ukraine zinatarajiwa kuzidisha mzozo wa uhakika wa chakula nchini Ethiopia. 

Huku zaidi ya robo tatu ya msaada wa WFP na ngano ya serikali  ambayo ni chakula kikuu nchini Ethiopia inatoka Ukraine au Urusi, hali ya hatari inatishia kusukuma juu gharama yake, pamoja na ile ya mbolea, hali ambayo iko nje ya uwezo wa mamilioni ya wakulima wa Ethiopia. 

Msafara wa WFP ukiwa na msaada wa vyakula kwa ajili ya watu Tigray Ethiopia na Afar.
WFP Ethiopia
Msafara wa WFP ukiwa na msaada wa vyakula kwa ajili ya watu Tigray Ethiopia na Afar.

Hatari ya kufunga shughuli za kibinadamu 

Zaidi ya hayo, ukata mkubwa wa fedha wa WFP umesababisha shirika hilo la Umoja wa Mataifa la kutoa misaada ya chakula kutahadharisha juu ya janga linalokuja la utapiamlo. 

Ufadhili wake wa kutibu zaidi ya wanawake na watoto milioni 1.4 wenye utapiamlo wa hali ya juu Kaskazini mwa Ethiopia unaisha haraka. 

Hadi sasa, ukosefu mkubwa wa fedha umewezesha oparesheni za WFP kutoa matibabu ya lishe kwa asilimia 40 pekee ya akina mama na watoto walioathirika kaskazini mwa Ethiopia kati ya Januari na Aprili.  

Hiyo ina maana watatibiwa 560,000 tu kati ya watu milioni 1.4 iliyolengwa. 

Na pengo hilo limelazimisha kupunguzwa kwa mgao kwa zaidi ya wakimbizi 700,000latika eneo hilo, ambao sasa wanapokea asilimia 50 tu ya mahitaji yao ya chini ya lishe. 

WFP inalenga kufikia zaidi ya watu milioni 11 walio hatarini zaidi katika kipindi cha miezi sita ijayo lakini inakabiliana na pengo kubwa la ufadhili la dola milioni 470.