Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Vifaa vya kupigia kura CAR vyawasili, MINUSCA yashiriki kwenye ulinzi 

Ujumbe wa Umoja wa Mataifa nchini Jamhuri ya Afrika ya kati ukiweka ulinzi kwenye makao makuu ya kusimamia uchaguzi.
MINUSCA/Francis Yanbedji
Ujumbe wa Umoja wa Mataifa nchini Jamhuri ya Afrika ya kati ukiweka ulinzi kwenye makao makuu ya kusimamia uchaguzi.

Vifaa vya kupigia kura CAR vyawasili, MINUSCA yashiriki kwenye ulinzi 

Amani na Usalama

Kuelekea uchaguzi wa rais na wabunge nchini Jamhuri ya Afrika ya Kati, CAR tarehe 27 mwezi huu wa Desemba, shehena ya vifaa vya uchaguzi vimewasili kwenye mji mkuu wa nchi hiyo Bangui ikiwa ni msaada kutoka Afrika Kusini na walinda amani wa Umoja wa Mataifa pamoja na serikali wanashirikiana kwenye ulinzi wa vifaa hivyo.

Vifaa hivyo ni pamoja na masanduku  12,000 ya kutumbukiza kura, vyumba 12,000 vya kupigia kura na makasha 4,200 ya makaratasi ya kupigia kura na shehena hiyo ilipokelewa kwenye uwanja wa ndege wa kimataifa wa M’poko mjini Bangui. 

Vifaa hivyo vitasambazwa katika majimbo mbalimbali ya taifa hilo na kwa kuzingatia hilo uhifadhi wake unahitaji ulinzi wa kutosha ambao unatolewa na polisi wa CAR kwa kushirikiana na walinda amani wa Umoja wa Mataifa kutoka Rwanda. 

Meja Vincent Ndayisaba ambaye ni kamanda wa kikosi cha Rwanda MINUSCA amesema, “kikosi cha Rwanda kama ilivyo vikosi vingine katika MINUSCA, kina jukumu adhimu la kulinda vifaa vya uchaguzi.  Na tunashirikiana hapa na polisi ili kuimarisha ulinzi wa vifaa hivi. Kwa  hiyo kazi yetu ni kulinda na kutambua walioko hapa. Polisi na walinda amani kutoka Rwanda tunafahamu lengo letu na tunapaswa kushirikiana na hakuna tatizo.” 

Nacho kituo cha kukusanya takwimu za kura kinahakikisha kiko tayari kuweza kupokea matokeo ya kura na inatumia vifaa vya mwaka 2015. 

Huguette Ndindy ni Mkurugenzi wa Takwimu katika Tume ya Uchaguzi CAR na anasema,  “Kituo cha takwimu za matokeo ya uchaguzi ni uti wa mgongo wa tume ya taifa ya uchaguzi. Kwa hiyo tangu mwak a2015 hadi leo ni vifaa hivyo hivyo vinatumika katika utambuzi wa maeneo, uandikishaji wapiga kura. Halikadhalika mitambo ya kupokea matokeo ya kura na mashine za kuchapishia ni ya zamani kwa hiyo ni vyema kutunza vyema vifaa hivyo.” 

Vifaa vya kupigia kura vinavyopaswa kusafirishwa majimboni, vitasafirishwa kwa njia ya anga na barabara siku chache zijazo.