Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Wanawake kuendelea kuteseka zaidi na athari za COVID-19 ikilinganishwa na wanaume: ILO

Mfanyakazi katika kiwanda cha mavazi nchini Nicaragua akikagua nguo
ILO Photo/Marcel Crozet
Mfanyakazi katika kiwanda cha mavazi nchini Nicaragua akikagua nguo

Wanawake kuendelea kuteseka zaidi na athari za COVID-19 ikilinganishwa na wanaume: ILO

Wanawake

Utafiti mpya ulifanywa na shirika la kazi la Umoja wa Mataifa ILO umeonesha ni wanawake wachache sana kati ya wengi waliopoteza ajira kutokana na athari za janga la Corona au COVID-19 watakaoweza kupata kazi ikilinganishwa na wanaume. 

Taarifa ya utafiti mpya uliofanywa na shirika hilo na kutangazwa leo huko Geneva, Uswisi imesema kumekuwa na upotevu mkubwa wa ajira, na mateso kwa wanawake katika kipindi cha janga hilo lakini bado wanawake wataendelea kuathirika. 

Utafiti umeonesha kati ya mwaka 2019 na 2020 ajira kwa wanawake zilipungua kwa asilimia 4.2 duniani, ikiwakilisha ajira milioni 54, wakati wanaume waliathirika kwa asilimia 3 au ajira milioni 60. 
Hii inamaanisha kutakuwa na upungufu wa wanawake milioni 13 katika ajira mwaka huu ikilinganishwa na mwaka 2019, ilihali idadi wa wanaume katika ajira inatarajiwa kuongezeka kwa viwango vilivyo onekana katika miaka miwili. 

Kwa maana nyingine ni kuwa asilimia 43 tu ya wanawake walio kwenye umri wa kuajiriwa ndio watakaopata ajira mwaka 2021, ikilinganishwa na asilimia 69 ya wanaume ambao wanatarajiwa kupata ajira mwaka huu. 

Utafiti huo umeonesha wanawake wamekuwa waathirika wakubwa kwenye ajira na kukosa kipato sababu maeneo wanayofanyia kazi ndio yameathirika zaidi na janga la Corona mfano kwenye sekta ya malazi, chakula na utengenezaji. 

Nchini Mongolia wanawake wawili wakiwa kiwandani
ILO Photo
Nchini Mongolia wanawake wawili wakiwa kiwandani


  Utofauti duniani

Sio kila bara limeshuhudia hali mbaya kwakufanana, kwa mfano, utafiti umeonesha ajira huko bara la Amerika zimeathirika vibaya, kiwango cha ajira kimeshuka kwa zaidi ya asilimia tisa. 
Hii inafuatiwa na nchi za kiarabu ambazo ajira zimeshuka kwa zaidi ya asilimia tisa, ikifuatiwa na bara la Asia – Pasifiki kwa asilimia 3.8. 
Bara la ulaya limeshuhudia anguko la ajira kwa asilimia 2.5, na Asia ya kati ikiwa na asilimia 1.9 ya kiwango cha ajira zilizopotea. 
Kwa upande wa Afrika, ajira kwa wanaume zimepungua kwa asilimia 0.1 kati ya mwaka 2019 na 2020, wakati ajira za wanawake zikipungua kwa asilimia 1.9. 

 

   Juhudi za kupambana na tatizo 

Wakati wote wa janga la Corona, wanawake waliweza kumudu vizuri katika nchi zilizochukua hatua madhubuti za kuwasaidia waliopoteza ajira na kuwaruhusu kurudi mapema iwezekanavyo katika katika kazi zao.
Kuna baadhi ya nchi mfano Chile na Colombia, ruzuku ya mshahara ilitolewa huku kiwango cha juu ya ruzuku wakipewa wanawake.
Na Colombia na Senegali zilikuwa miongoni mwa nchi zilizotengeneza au kuimarisha usaidizi kwa wanawake wajasiriamali. 
Wakati huo huo, Mexico na Kenya kuliweka upendeleo maalum katika kuhakikisha wanawake wananufaika na ajira kwenye mipango ya umma.