Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

UN imejipanga kuwa na uwiano wa kijinsia kwenye uongozi hadi mashinani

Katibu Mkuu wa UN António Guterres (wa 2 kutoka kulia mstari wa mbele) akiwa na wanawake viongozi walio kwenye jopo la viongozi waandamizi kabisa wa UN, hatua ambayo inadhihirisha kauli yake ya kutekeleza usawa wa jinsia kwa vitendo.
UN /Mark Garten
Katibu Mkuu wa UN António Guterres (wa 2 kutoka kulia mstari wa mbele) akiwa na wanawake viongozi walio kwenye jopo la viongozi waandamizi kabisa wa UN, hatua ambayo inadhihirisha kauli yake ya kutekeleza usawa wa jinsia kwa vitendo.

UN imejipanga kuwa na uwiano wa kijinsia kwenye uongozi hadi mashinani

Wanawake

Umoja wa Mataifa utaendelea na hatua zake za kuhakikisha kuna uwiano wa kijinsia kwenye ngazi za uongozi siyo tu katika nafasi andamizi za juu kama ambavyo imekamilisha hivi sasa bali pia kwenye ofisi za mashinani ambako bado kuna changamoto.

Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterres amesema hayo leo akihutubia mkutano wa uwiano wa kijinsia kwenye uongozi, mkutano ulioandaliwa kikundi cha marafiki wa uwiano wa kijinsia kinachoongozwa na Qatar na Rwanda.

Mkutano huo wa kikundi hiki hufanyika wakati wa mwezi Machi ambao ni mwezi wa wanawake unaoanza na maadhimisho ya siku ya wanawake duniani.

Sekretarieti tunasonga mbele

Guterres amesema “hii leo naweza kujivunia kuwa tunaelekea kufikia usawa wa kijinsia kwenye uongozi katika mfumo mzima wa Umoja wa Mataifa. Tumefiia usawa katika uongozi andamizi miaka miwili kabla ya kipindi tulichojiwekea. Nazungumzia tuna viongozi 190 waandamizi.”
 
Amefafanua kuwa katika Sekretarieti, uwiano wa wanawake katika ngazi ya ueledi hadi juu  imeongezeka kutoka asilimia 37 mwaka 2017 hadi zaidi ya asilimia 42 mwaka 2021. Amesema mafanikio hayo yamepatikana licha ya ukata unaokumba shirika, hali inayofanyika kwa kulazimu kusitisha ajira ya kawaida. 

Bintou Keita kutoka Guinea, ni Mwakilishi Maalum wa Katibu Mkuu wa UN nchini DRC na Mkuu pia wa MONUSCO
N /Eskinder Debebe
Bintou Keita kutoka Guinea, ni Mwakilishi Maalum wa Katibu Mkuu wa UN nchini DRC na Mkuu pia wa MONUSCO

“Kwa mwelekeo huu, Sekretarieti ya Umoja wa Mataifa inaweze kufikia uwiano wa kijinsia kwenye uongozi katika robo ya pili yam waka 2027, kabla ya lengo la mwaka 2028 tulilojiwekea,” amesema Guterres.

Bado kuna changamoto kufikia uwiano wa usawa ofisi za mashinani

Ingaw kuna mafanikio kwenye makao makuu ya UN, maendeleo mashinani yamekuwa ya “mwendo wa Kobe” na bila usawa.

Mwaka 2006 kulikuwa na mwanamke 1 tu akiongoza ofisi za mashinani sasa idadi ni 16- António Guterres, Katibu Mkuu UN

Katika operesheni za ulinzi wa amani, asilimia 32 ya wafanyakazi raia ni wanawake ilhali wanaume ni asilimia 68. Hata angalau ni maendeleo kidogo kwa kuwa mwaka 2017 wafanyakazi raia wanawake walikuwa ni asilimia 28 pekee.

Ofisi hizi za ulinzi wa amani zitanufaika zaidi kwa kuwa na wanawake watendani, “hivyo tunapaswa kuweka mazingira bora ya kufanya kazi na ya kuishi ili wanawake wawe na ushiriki sawa na ambayo yanaweza kukidhi mahitaji ya wanawake.”

Nimechukua hatua 

Katibu Mkuu amesema kwa yeye binafsi amechukua hatua ya kuongeza usawa kwenye ngazi ya uongozi ambapo mwaka 2017 alitoa wito wa kuwasilisha majina ya watu watakaoshika nafasi ya wawakilishi maalum wa Umoja wa Mataifa mashinani.

“Hadi leo nimepokea Zaidi ya majina 700 kutoka nchi wanachama, mashirika na watu binafsi na katika hayo asilimia 40 ni wanawake, amao nudu yao wanatoka nchi za kusini. Nimechagua 25 kuwa wakuu au wasaidizi wa ofisi za UN mashinani na kati ya hao wanawake ni 16.”

Ni maendeleo makubwa kwa kuwa mwaka 2006 kulikuwa na mwanamke mmoja tu akiongozi ofisi zetu za mashinani.

HAtua ya pili amesema ni ufuatiliaji wa uajiri ambapo amesema kuna kanuni za kutaka mameneja wanaoajiri kupatia kipaumbele wanawake iwapo wanakuwa na sifa.

“Kanuni hii imekuweko kwa zaidi ya miaka 20 lakini haitekelezwi kwa kuwa kulikuwa hakuna mbinu ya kuwawaijbisha. Sasa mameneja waandamizi wanawajibishwa na uamuzi wao wa kuajiri na ofisi yangu inafuatilia utekelezaji.” Amesema Katibu Mkuu.

Amesema hatua ya tatu ni kuanza kubaini wanawake wenye sifa ambao watajaza nafasi za wafanyakazi tarkribani 4000 wanaotarajiwa kustaafu katika kipindi cha miaka 9 ijayo, wengi wao wakiwa wanaume.

Hatua hizo ni pamoja na kuweka jukwaa la watendaji wa ndani wenye vipaji.

“Nafahamu kuna hofi kutoka kwa baadhi ya nchi wanachama kuwa uwiano wa kijinsia kwenye uongozi, unaweza kufuta hoja ya uwakilishi wa kijiografia kwenye uajiri, la hasha! Naweza kuwahakikishia kuwa tunazingatia malengo yote mawili, jinsia na jiografia,” ametanabaisha Guterres.