Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

COVID-19 yachochea madhila ya ukatili dhidi ya wanawake :UN WOMEN

Jijini Dar es Salaam, Tanzania , wanafunzi wasichana wakiwa kwenye maandamano yaliyoandaliwa kupinga ukatili kijinsia
UN Women Tanzania/Deepika Nath
Jijini Dar es Salaam, Tanzania , wanafunzi wasichana wakiwa kwenye maandamano yaliyoandaliwa kupinga ukatili kijinsia

COVID-19 yachochea madhila ya ukatili dhidi ya wanawake :UN WOMEN

Wanawake

Ripoti mpya iliyotolewa na Shirika la wanawake la Umoja wa Mataifa UN Women iliyoangazia athari za janga la COVID-19 kwa usalama wa wanawake nyumbani na katika maeneo ya umma imeonesha kuwa hisia za usalama za wanawake zimepotea, na kusababisha athari mbaya kwa hali yao ya kiakili na kimihemko.

Ripoti hiyo iliyotolewa leo ikiwa ni siku moja kabla ya siku ya Kimataifa ya kutokomeza ukatili dhidi ya wanawake Novemba 25 wakati ambao dunia inaanza Siku 16 za uchagizaji wa kupinga Ukatili wa Kijinsia.

Mkurugenzi Mtendaji wa UN WOMEN Sima Bahous amesema unyanyasaji dhidi ya wanawake ni mgogoro uliopo wa kimataifa ambao unastawi kutokana na kuwepo kwa migogoro mingine duniani. Migogoro ya  majanga ya asili yanayohusiana na mabadiliko ya tabianchi, ukosefu wa uhakika wa chakula na ukiukaji wa haki za binadamu vyote huchangia wanawake na wasichana kuishi katika hali ya hatari, hata katika nyumba zao na jamii zao. 

“Janga la coronavirus">COVID-19, ambalo lililazimu kutengwa na kutengwa kwa jamii, liliwezesha kuzuka kwa  janga la pili, kivuli la ukatili dhidi ya wanawake na wasichana, ambapo mara nyingi walijikuta wamefungwa na wanyanyasaji wao. Takwimu zetu mpya zinasisitiza udharura wa juhudi za pamoja kukomesha hili,” amesema Bahous.

Maadhimishoya siku 16 za kupinga ukatili yanafanyika kuanzia tarehe 25 Novemba hadi 10 Desemba, chini ya kaulimbiu ya kimataifa iliyowekwa na Kampeni ya UNiTE ya Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa, “Orange the World: Tokomeza Ukatili dhidi ya Wanawake Sasa! ”

Tokomeza ukatili dhidi ya wanawake
UNTF
Tokomeza ukatili dhidi ya wanawake

Kilichobainika kwenye ripoti

Ripoti hiyo imeonesha karibu mwanamke 1 kati ya 2 aliripoti kwamba yeye au mwanamke anayemjua alikumbwa na hali fulani ya ukatili tangu kuzuka kwa janga la COVID-19 lianze. Wanawake ambao waliripoti hali hii walikuwa na uwezekano mara 1.3 zaidi wa kuripoti kuongezeka kwa athari kiakili na mihemko kuliko wanawake ambao hawakuripoti.

Matokeo hayo pia yamefichua kuwa takriban mwanamke 1 kati ya 4 anahisi kuwa salama nyumbani huku migogoro iliyopo imeongezeka ndani ya kaya tangu janga hili lianze.

Wanawake walipoulizwa kwa nini walijihisi kutokuwa salama nyumbani, wametaja unyanyasaji wa kimwili kuwa mojawapo ya sababu (21%). Baadhi ya wanawake waliripoti haswa kwamba waliumizwa na wanafamilia wengine (21%) au kwamba wanawake wengine wanaowafahamu  katika kaya walikuwa wakiumizwa (19%).

Kwa upande wa nje ya nyumba zao, wanawake pia wanahisi kuathiriwa zaidi na dhuluma, huku 40% ya waliohojiwa wakisema wanahisi salama kidogo kutembea peke yao usiku tangu kuanza kwa COVID-19. 

Takriban wanawake 3 kati ya 5 pia wanafikiri kuwa unyanyasaji wa kijinsia katika maeneo ya umma umezidi kuwa mbaya wakati wa janga la COVID-19.

Waweza kusoma ripoti kamili hapa 

Mwanamke wa Sudan Kusini ambaye alipigwa na mume wake anatafuta hifadhi katika nyumba ya kaka yake
© UNICEF/Albert Gonzalez Farran
Mwanamke wa Sudan Kusini ambaye alipigwa na mume wake anatafuta hifadhi katika nyumba ya kaka yake

Kauli ya Katibu Mkuu wa UN

Katika taarifa yake kwa vyombo vya habari Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterres amesema unyanyasaji dhidi ya wanawake na wasichana umeendelea kuwa suala linaloenea na linaloonesha ukiukwaji wa haki za binadamu duniani leo.

Amesema suala hilo ni uhalifu wa kuchukiza na ni dharura ya afya ya umma, yenye madhara makubwa kwa mamilioni ya wanawake na wasichana katika kila kona ya dunia. Ameeleza takwimu zilizotolewa na UN Women zinathibitisha kwamba wakati wa janga la COVID-19, viwango vya ukatili dhidi ya wanawake na wasichana vimeongezeka.

“Unyanyasaji dhidi ya wanawake hauepukiki. Sera na mipango sahihi huleta matokeo. Hiyo ina maana ya kuwa mikakati ya kina, ya muda mrefu ambayo inakabiliana na visababishi vikuu vya unyanyasaji, kulinda haki za wanawake na wasichana, na kukuza vuguvugu dhabiti na linalojitegemea la haki za wanawake. Mabadiliko yanawezekana, na sasa ni wakati wa kuongeza juhudi zetu ili kwa pamoja tuweze kutokomeza ukatili dhidi ya wanawake na wasichana ifikapo mwaka 2030,” amesisitiza Katibu Mkuu Guterres.

Wito wa wataalamu 

Wataalam wa Umoja wa Mataifa na wale wa kikanda wametoa wito kwa mataifa yote ulimwenguni kufanya bidii ipasavyo na kuondoa vipingamizi vinavyokwamisha usawa wa kijinsia.

Taarifa ya wataalamu hao iliyotolewa leo mjini Geneva Uswisi imesema wanawake na wasichana kila mahali wanaendelea kukabiliwa na aina nyingi za ukatili wa kijinsia, ikiwa ni pamoja na mauaji ya wanawake, ukatili mtandaoni na unkatili wa majumbani.