Pombe yahusishwa na wagonjwa wapya wa saratani 740,000 mwaka 2020 

14 Julai 2021

Habari mpya kuhusu ugonjwa wa saratani inasema kwamba pombe imebainika kuwa kisababishi cha wagonjwa wapya 740,000 wa saratani au kansa kwa mwaka jana wa 2020. Takwimu  hizo ni za ulimwengu mzima na zimetolwa na taasisi ya kimataifa ya utafiti wa saratani, IARC, ambayo ni taasisi tanzu ya shirika la Umoja wa Mataifa la afya ulimwenguni, WHO. 

Kupitia chapisho la Lancet Oncology, wanasayansi wa IARC wametoa takwimu zinazoonesha kwamba ingawa mwenendo wa unywaji pombe kupindukia ambao ni sawa na zaidi ya chupa mbili kwa siku ulisababisha asilimia 86 ya wagonjwa wote wapya, unywaji wa kiwango cha kati ambao ni hadi chupa mbili kwa siku, nao pia ulisababisha zaidi ya wagonjwa wapya laki moja wa saratani duniani kote. 

Mtafiti kutoka taasisi hiyo Harriet Rumgay amenukuliwa katika taarifa yo iliyotolewa leo huko Lyon, Ufaransa akisema “makadirio haya yanatupatia taswira ya mzigo wa saratani utokanao na unywaji pombe, takwimu ambazo zimechambuliwa kijinsia, kinchi na kimaeneo. Tumeweza pia kupata idadi ya wagonjwa wapya wa saratani wakihusishwa na hata unywaji mdogo au wa kati wa pombe na hii imeonesha athari za pombe katika kuongeza idadi ya wagonjwa wa saratani.”

Uchambuzi wa takwimu huo kijinsia unaonesha kuwa katika idadi hiyo, wanaume ni 567,000 sawa na robo tatu ya wagonjwa wote wapya.

Taasisi hiyo inasema kuwa unywaji wa pombe unaongeza hatari ya saratani katika maeneo saba ikiwemo mdomo, njia ya mfumo wa chakula, utumbo mpana na matiti kwa upande wa wanawake.

Ka mujibu wa takwimu hizo, saratani ambayo ilikuwa na wagonjwa wengi zaidi miongoni mwa ile iliyosababishwa na unywaji pombe ni saratani ya mfumo wa kupokea chakula, ikifuatiwa n aini, na matiti.
 
Dkt. Isabelle Soerjormataram kutoka IARC, amesema unywaji pombe unaongeza kwa kiasi kikubwa mzigo wa saratani duniani “lakini mara nyingi athari ya pombe kwa saratani inapuuzwa. Hii inaangazia umuhimu wa kutekeleza sera nah atua za kuongeza uelewa wa umma juu ya uhusiano kati ya unywaji pombe na hatari ya kupata saratani.”

 

♦ Kurambaza ukurasa mahsusi wa Siku ya Kiswahili Duniani bofya  hapa.
♦ Iwapo ungependa kupokea taarifa kutoka UN News Kiswahili kila wakati zinapochapishwa jisajili  hapa.
♦ Pia unaweza kupakua apu ili kusikiliza matangazo yetu wakati wowote popote ulipo.
♦ Tembelea pia chaneli yetu ya Youtube na pia Soundcloud na Twitter