WHO yaorodhesha hatua za kuokoa watu milioni 7 za kuepukana na saratani

4 Februari 2020

Katika maadhimisho ya siku ya saratani duniani hii leo, Shirika la Afya Ulimwenguni, WHO limeelezea umuhimu wa kuongeza huduma za kukabiliana na saratani katika nchi zenye kipato cha chini na cha wastani.

WHO imeonya kwamba, ikiwa hali ya sasa itaendelea, ulimwengu utashuhudia ongezeko la asilimia 60 la visa vya saratani katika miongo miwili ijayo. Ongezeko kubwa zaidi takriban asilimia 81 ya visa vipya vitatokea katika nchi zenye kipato cha chini na cha wastani, ambapo viwango vya kuishi kwa sasa viko chini sana.

 Hii ni kwa sababu nchi hizi kwa muda zimelazimika kuwekeza rasilimali kidogo za kiafya katika kupambana na magonjwa ya kuambukiza na kuimarisha afya ya mama na mtoto, wakati huduma za afya hazina vifaa vya kuzuia, kugundua na kutibu saratani. Mnamo mwaka wa 2019, zaidi ya asilimia 90 ya nchi zenye kipato cha juu ziliripoti kuwa huduma kamili za matibabu ya saratani zinapatikana katika mfumo wa afya ya umma ikilinganishwa na chini ya aslimia 15 katika nchi zenye kipato cha chini.

Akizungumzia ripoti hiyo Dk.Ren Minghui, Mkurugenzi Mkuu Msaidizi, huduma ya afya kwa wote na magonjwa yanayoambukizwa na yasiyoambukiza amesema, “huu ni wito kwa wote kushugulukia tofauti za usawa kati ya huduma za sratani katika nchi tajiri na zile masikini.”

Ameongeza kuwa, “iwapo watu wanapata huduma za msingi na mifumo ya uhamishaji basi saratani inaweza kugundulika mapema, kutibiwa vizuri na kupona. Saratani haipaswi kuwa adhabu ya kifo kwa mtu yeyote, mahali popote. "

Mkurugrnzi Mkuu wa WHO, Dk Tedros Adhanom Ghebreyesus amesema, “angalau maisha ya watu  milioni 7 yangeokolewa katika kipindi cha muongo mmoja ujao, kwa kutambua sayansi inayofaa kwa hali ya kila nchi, kwa kushugulukia saratani kupitia mifumo ya afya ya umma kwa wote na kwa kuhamasisha wadau mbali mbali kufanya kazi kwa pamoja.”

WHO imeorodhesha hatua kadhaa za kuthibitika kuzuia visa vipya vya saratani. Hii ni pamoja na kudhibiti utumiaji wa tumbaku, inayosababisha asilimia 25 ya vifo vya saratani, chanjo dhidi ya homa ya ini aina B kwa ajili ya kuzuia saratani ya ini, kutokomeza saratani ya shingo ya uzazi kwa kupata chanjo dhidi ya HPV, uchunguzi na matibabu, kutekeleza ufuatiliaji wa saratani wenye tija na unaohakikisha ufikiaji wa matunzo pamoja na misaada ya maumivu.

 WHO imesema kila serikali ina wajibu wa kuchagua matibabu ya saratani yanayofaa, wakati ikigundua kuwa tiba zilizoanzishwa, ambazo nyingi ni nzuri na zina bei nafuu, zinaweza kutoa faida vita dhidi ya saratani kwa gharama ya chini.

 

TAGS: WHO, saratani, Dk Tedros Adhanom Ghebreyesus

 

♦ Tafadhali iwapo unataka kupokea taarifa kutoka UN News Kiswahili kila wakati zinapochapishwa jisajili  hapa.
♦ Pia unaweza kupakua apu ili kusikiliza matangazo yetu wakati wowote popote ulipo.
♦ Tembelea pia chaneli yetu ya Youtube na pia Soundcloud