Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Tukiwa na ufadhili wa kuaminika tutaokoa maisha ya mamilioni-WFP

Wananchi wa Haiti wakiwa wamepanga foleni kupokea msaada wa chakula kutoka WFP kwenye kitongoji cha Chansolme kilichopo wilaya ya Kaskazini-Magharibi mwa Haiti.
WFP/Alexis Masciarelli
Wananchi wa Haiti wakiwa wamepanga foleni kupokea msaada wa chakula kutoka WFP kwenye kitongoji cha Chansolme kilichopo wilaya ya Kaskazini-Magharibi mwa Haiti.

Tukiwa na ufadhili wa kuaminika tutaokoa maisha ya mamilioni-WFP

Msaada wa Kibinadamu

Shirika la Umoja wa Mataifa la mpango wa chakula WFP limesema kuwepo kwa ufadhili wa kutosha, wa wakati na wa kuaminika inaamanisha shirika hilo litaweza kuamua wapi na jinsi gani fedha zitumike ili kuokoa maisha ya mamilioni ya watu duniani.

Kwa mujibu wa mkurugenzi mtendaji wa WFP David Beasley hali hiyo itawapatia fursa ya kuchukua hatua haraka kunakohitajika kushughulikia mahitaji na dharura za kiwango kikubwa kote duniani na pia inaliruhusu shirika hilo kufadhili migogoro iliyopuuzwa pamoja na kufikisha msaada muhimu wa chakula kwa wale wanaohitaji haraka. “Upatikanaji rahisi wa fedha unaturuhusu kuwa na ufanisi na mpangilio katika kazi zetu. Tunaweza kuchukua hatua haraka zaidi, kuokoa gharama na kuhakikisha thamani ya kila dola tunayopokea. Kwa kifupi, njia hii ya ufadhili inamaanisha kuwa tunaweza kuokoa na kubadilisha maisha zaidi kila mwaka”

Bwana Beasely akitoa ombi la ufadhili zaidi amesema kiwango cha fedha za ufadhili kwenye shirika la WFP kinapungua na kinawakilisha asilimia tano tu ya jumla ya rasilimali zote lilizopewa shirika hilo kwa mwaka 2019.

Ameongeza kuwa kushuka kwa kiwango hicho cha ufadhili kunakwenda kinyume na mkataba  ujulikanao kama “Grand Bargain” ambao ulipitishwa kwenye mkutano wa dunia wa masuala na misaada ya kibinadamu mwaka 2016.

Amefafanua kwamba katika mkutano huo wahisani wa serikali waliahidi kuendelea kuongeza ufadhili kwa masuala ya kibinadamu ili kufikia lengo la kimataifa la asilimia 30 ya ufadhili wa kibinadamu ifikapo mwaka 2020.

Bwana Beasley wamewasihi wahisani kote duniani kuendelea kunyoosha mkono na kutoa fedha hizo akisema bila ufadhili huo Maisha ya mamilioni ya watu walio katika dharura za kibinadamu yatakuwa njiapanda.