Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

UNICEF yawezesha wakazi wa Goma nchini DRC kunywa maji masafi

Vituo vya maji vilivyowekwa na UNICEF kwa wakazi waliopoteza makazi  yao kufuatia mlipuko wa volkano ya Nyiragongo huko Sake jimboni Kivu Kaskazini.
UNICEF/Jean-Claude Wenga
Vituo vya maji vilivyowekwa na UNICEF kwa wakazi waliopoteza makazi yao kufuatia mlipuko wa volkano ya Nyiragongo huko Sake jimboni Kivu Kaskazini.

UNICEF yawezesha wakazi wa Goma nchini DRC kunywa maji masafi

Msaada wa Kibinadamu

Shirika la Umoja wa Mataifa la kuhudumia watoto, UNICEF linahaha kurejesha huduma ya maji safi na salama kwa wakazi 200,000 wa mjji wa Goma jimboni Kivu Kaskazini nchini Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo, DRC baada ya huduma hiyo kuharibiwa na mlipuko wa volkano kwenye mlima Nyiragongo tarehe 22 mwezi uliopita wa Mei.
 

Taarifa ya UNICEF iliyotolewa leo mjini Goma inasema, “miongoni mwa watu hao 200,000 kuna watoto 100,000 katika mji huo ulioko mashariki mwa DRC. Mlipuko wa Volkano uliyeyusha mabomba makuu ya kusambaza maji na kuharibu tanki la kuhifadhi maji la mita za ujazo 5000.”

Mtaalamu wa masuala ya dharura wa UNICEF Hye Sun amesema bila maji safi na salama, watoto na familia zao wako hatarini kukumbwa na magonjwa ya kuambukizwa kutokana na maji machafu kama vile kipindupindu.

“Kipindupindu ni hatari sana kwa watoto, wazee na wenye utapiamlo kwa hiyo mlipuko wa kipindupindu hapa utakuwa na madhara makubwa kwa watoto.” amesema mtaaamu huyo akiongeza kuwa watoto wenye umri wa chini ya miaka 5 wanakumbwa zaidi na ugonjwa huo na wako hatarini zaidi kufariki dunia, “kwa hiyo ni vyema turudishe maji haraka iwezekanavyo.”

Ambacho UNICEF inafanya sasa ni kushirikiana na wadau wa kitaifa na kimataifa ikiwemo Regideso, ambalo ni shirika la maji nchini humo katika kupitisha maeneo mapya mabomba hayo ili hatimaye maji yaweze kusafirishwa kutoka Ziwa Kivu kuingia katika mfumo wa maji.

Kutokana na mfumo huo, idadi ya wilaya zisizo na maji zimepungua kutoka 12 hadi 4 na “matarajio ni kwamba matengenezo yakikamilika mwishoni mwa wiki, ni wilaya 2 tu zitasalia bila maji.”

UNICEF imefunga vituo 15 vya dharura vya kuweka dawa ya kutakatisha maji karibu na Ziwa Kivu ambako wafanyakazi wanaweka vidonge hivyo kwenye madumu ya maji yanayotumiwa na wakazi wa eneo hilo kuteka maji kutoka ziwani na hivyo kuhakikisha maji ni salama kwa kunywa.