Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Hofu ya kulipuka tena volkano Nyiragongo yafurusha maelfu Goma 

Shule zilizoharibiwa katika jimbo la Kivu Kaskazini nchini DRC baada ya mlipuko wa volkano ya mlima Nyiragongo tarehe 22 mwezi Mei mwaka 2021. Shule ziko katika vijiji vya Buhene na Mujoga, takribani kilometa 7 kutoka mlima Nyiragongo.
© UNICEF/Jospin Benekire
Shule zilizoharibiwa katika jimbo la Kivu Kaskazini nchini DRC baada ya mlipuko wa volkano ya mlima Nyiragongo tarehe 22 mwezi Mei mwaka 2021. Shule ziko katika vijiji vya Buhene na Mujoga, takribani kilometa 7 kutoka mlima Nyiragongo.

Hofu ya kulipuka tena volkano Nyiragongo yafurusha maelfu Goma 

Msaada wa Kibinadamu

Maelfu ya wakazi wa mji wa Goma ulioko jimbo la Kivu Kaskazini nchini Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo, DRC hawana makazi hivi sasa na wako kwenye harakati za kuhama hata kule walikokimbilia karibu na mji huo bada ya mamlaka kuwaagiza wahame kwa hofu ya kwamba volkano katika Mlima Nyiragongo inaweza kulipulka tena. 

Ofisi ya Umoja wa Mataifa wa uratibu wa misaada ya kibinadamu, OCHA amri ya kuhama ilitolewa usiku wa tarehe 26 mwezi huu wa Mei, na Gavana wa jimbo hilo la Kivu Kaskazini ambaye ametaka wakati katika wilaya 10 wahame kama njia ya kujihami iwapo volkano hiyo italipuka. 

Msemaji wa OCHA, Jens Laerke akizungumza na waandishi wa habari hii leo mjini Geneva, Uswisi amesema bado haifahamiki idadi ya watu waliokimbia mji huo wa Goma hivi sasa, lakini takribani watu 400,000 watakuwa wamekumbwa na agizo hilo la kuhama. 

“Misururu mirefu ya magari ilishuhudiwa jana Alhamisi kwenye barabara kuu ya kutoka mji wa Goma. Watu wanaelekea maeneo tofauti tofauti wengi wao kwa miguu, wakiwa na virago wanavyoweza kubeba. Wengine pia wanahama kwa kutumia magari na boti,” amesema Bwana Laerke. 

Watu wanaondoka kutoka maeneo waliyohamishiwa awali na sasa mwelekeo wao ni Sake huko Goma Magharibi, Rwanda upande wa Mashariki na Rutshuru upande wa Kaskazini wakivuka Ziwa Kivu kwa boti hadi mji wa Bukavu ulioko jimbo la Kivu Kusini. 

Mlipuko wa kwanza uliotokea tarehe 22  mwezi huu wa Mei ulisababisha vifo vya watu 32 na kituo cha ufuatiliaji wa Volkano kilichoko Goma kimeonya kuwa kuna hatari ya mlipuko mwingine kutokea. 

Hadi jana mitetemo yenye nguvu ilisikika ambapo moja ya mitetemo hiyo ilikuwa na ukubwa wa 4.9 katika kipimo cha richa. 

Kwa mujibu wa wataalamu, mitetemo kama hiyo inaweza kusababisha lava zaidi kutoka kupitia kwenye nyufa za mlima. 

Mlipuko huo wa takribani wiki moja iliyopita, ulisababisha lava, majivu na hewa kutoka kwenye mlima huo kuharibu shule, vituo vya afya, huku miundombinu ya maji na umeme ikiharibiwa sambamba na barabara. 

Kwa sasa mji wa Goma na viunga vyake hauna maji, na kutokana na mwelekeo wa sasa wa watu kukimbia, tathmni mpya inafanyika leo huko Sake, Rutshuru na maeneo mengine wanayokimbilia ili kufahamu kiwango cha mahitaji. 

Tayari OCHA imeimarisha uwepo wake Goma ambako imetuma kikundi cha watu 8 kusaidia operesheni zake.