Zaidi ya watoto 170 wanahofiwa kupotea kufuatia mlipuko wa volkano Goma, DRC 

23 Mei 2021

Shirika la Umoja wa Mataifa la Kuhudumia Watoto, UNICEF, leo Jumapili limesema kwamba mamia ya watoto na familia katika mjini Goma nchini Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo, DRC wako katika hatari kufuatia mlipuko wa volkano wa Mlima Nyiragongo. 

Jana Jumamosi, anga la Goma liligeuka kuwa jekundu na lava ya volcano ikatoka katika mlima na kusababisha maelfu kukimbia mji wenye wakazi takribani milioni mbili. Ripoti za habari zinaonesha watu watano wanaweza kuwa wamefariki dunia wakati wa uokoaji, na nyumba nyingine zimeripotiwa kuharibiwa kabisa kaskazini mwa Goma. 

UNICEF inasema kuwa zaidi ya watoto 150 wametenganishwa na familia zao na zaidi ya watoto 170 wanahofiwa kutoweka. 

Zaidi ya watu 5,000 walivuka mpaka kuingia Rwanda kutoka Goma wakati lava inayokwenda polepole ilipokuwa ikisambaa kutoka kwenye mlima, na takribani watu 25,000 wamehama makazi yao huko Sake, kilomita 25 kaskazini magharibi mwa Goma, imesema UNICEF. 

"Hata hivyo, watu wengi taratibu wanarejea nyumbani kwani lava imeacha kutiririka asubuhi ya leo", imesema taarifa kwa vyombo vya habari ikieleza kuhusu wasiwasi kuwa mamia wanarudi na kukuta nyumba zimeharibiwa, na usambazaji wa maji na umeme vimevurugika sana. 

Bado haijafahamika ni kaya ngapi zimeathiriwa na mlipuko huo, inaeleza UNICEF, na kwamba makundi ya watoto katika eneo karibu na uwanja wa ndege wa Goma wameachwa bila makao na maskini. 

Timu ya UNICEF imepelekwa katika maeneo yaliyoathirika ya Sake, Buhene, Kibati na Kibumba ili kusughulikia mahitaji ya haraka, ambayo ni pamoja na kuweka vituo vya maji yenye klorini ndani na karibu na Sake ili kuzuia kuenea kwa kipindupindu. 

Shirika hilo linaimarisha ufuatiliaji wa ugonjwa hatari unaosababishwa na maji, hasa huko Goma kufuatia kurudi kwa wakazi. 

Vituo viwili vya muda vinaanzishwa kwa ajili ya watoto ambao hawajaambatana na yeyote au wametenganishwa na jamaa zao.  

UNICEF inasema itashirikiana na wadau wake kushughulikia visa vyovyote vya unyanyasaji wa kijinsia au unyanyasaji mwingine, ili kutoa msaada wa kutosha wa matibabu na kisaikolojia. 

MONUSCO ‘inafuatilia kwa karibu’ 

Ujumbe wa Umoja wa Mataifa wa kulinda amani nchini Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo, DRC, MONUSCO, umeandika katika tweeter mapema Jumapili kwamba helikopta kutoka katika ujumbe huo zilifanya safari juu ya kreta, na "ilikuwa ikifuatilia kwa karibu hali hiyo." 

Mara ya mwisho Nyiragongo kulipuka mnamo 2002, zaidi ya watu 100,000 walibaki bila makazi na karibu watu 250 waliripotiwa kufariki dunia. Ni moja ya volkano hai na zenye mlipuko mbaya zaidi.  

 

 

♦ Kurambaza ukurasa mahsusi wa Siku ya Kiswahili Duniani bofya  hapa.
♦ Iwapo ungependa kupokea taarifa kutoka UN News Kiswahili kila wakati zinapochapishwa jisajili  hapa.
♦ Pia unaweza kupakua apu ili kusikiliza matangazo yetu wakati wowote popote ulipo.
♦ Tembelea pia chaneli yetu ya Youtube na pia Soundcloud na Twitter