Poleni DRC kwa janga la mlipuko wa volkano Mlima Nyiragongo- Guterres
Poleni DRC kwa janga la mlipuko wa volkano Mlima Nyiragongo- Guterres
Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterres ameeleza masikitiko yake kufuatia vifo, majeruhi na uharibifu wa mali uliosababishwa na mlipuko wa volkano katika mlima Nyiragongo, huko Goma jimbo la Kivu Kaskazini nchini Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo, DRC.
Msemaji wa Umoja wa Mataifa Stephane Dujarric akizungumza na waandishi wa habari hii leo jijini New York, Marekani amesema, “Katibu Mkuu anatuma salamu za rambirambi kwa familia za walioathiriwa na janga hilo, pamoja na serikali na wananchi wa DRC. Hofu yetu ni kwamba janga hili linakuja wakati kuna ongezeko tayari la mahitaji ya kibinadamu kwenye eneo hilo yanayochochewa na ukosefu wa usalama na hali ngumu ya kiuchumi.”
Bwana Dujarric amesema kwa mujibu wa wafanyakazi wa Umoja wa Mataifa nchini DRC, watu 13 wamekufa kutokana na mlipuko huo wa volkano katika mlima Nyiragongo na watu wengine wapatao 5,000 wamepoteza makazi yao.
Katibu Mkuu wa #UN @antonioguterres asikitishwa na vifo na uharibifu wa mali uliosabaibshwa na mlipuko wa volkano ya mlima #Nyiragongo nchini #DRC #NyiragongoEruption https://t.co/rtQnMZz8V5
HabarizaUN
“Kama mnavyoweza kufikiria, idadi hiyo inaweza kubadilika kwa kuwa tunaendelea kupokea taarifa. Baada ya mlipuko, watu wengi walikimbilia huko Sake jimboni Kivu Kaskazini na wengine kuelekea Rwanda,” amesema Bwana Dujarric.
Kwa sasa barabara kati ya Rutshuru na Goma jimboni Kivu Kaskazini imefungwa, “na ni muhimu kutambua kuwa barabara hii ndio njia ya msingi ya kupeleka chakula mjini Goma. Njia za umeme na mabomba ya maji yameharibiwa na hivyo watu 500,00 hawana huduma ya maji na umeme.”
MONUSCO iko makini
Ujumbe wa Umoja wa Mataifa wa kulinda amani nchini DRC, MONUSCO nao uko makini kufuatilia hali ilivyo ambapo, “wakati wa mlipuko, helikopta ya MONUSCO ikiwa imebeba wataalam wa volkano iliruka kwenye mazingira ya mlima Nyarugongo na viunga vyake kutathmini hali ilivyo hususan ya kusambaa kwa lava. “
Kwa mujibu wa Dujarric, lava ilisambaa hadi Munigi, ambako ni kilometa 5 kaskazini -mashariki mwa Goma ikiwa ni karibu na uwanja wa ndege ambao bado umefungwa.
Kufungwa kwa uwanja huo wa ndege kunakwamisha misafara ya watoa misaada ya kibinadamu na walinda amani.
Kwa sasa watu waliokimbia wameanza kurejea makwao ingawa mitetemo bado inaripotiwa kwenye eneo hilo, huku walinda amani wakijiandaa kuondoa takataka kwenye barabara kuu kuelekea Goma pindi hali itakaporuhusu.
Tathmini ya haraka inaendelea kufahamu mahitaji ya kibinadamu ili hatimaye kusaidia serikali katika kusambaza huduma za msingi kama vile maji, malazi, huduma za afya na kuunganisha familia, hasa wakati huu ambapo yaelezwa watoto makumi kadhaa wamepotezana na familia zao.