Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu
Wanawake wa Afghanistan wakitembea Kishm kijijini Badakshan

Tusisahau kuwasaidia Waafghanistan na jamii zinazowapa hifadhi: UNHCR

UNAMA/Torpekai Amarkhel
Wanawake wa Afghanistan wakitembea Kishm kijijini Badakshan

Tusisahau kuwasaidia Waafghanistan na jamii zinazowapa hifadhi: UNHCR

Msaada wa Kibinadamu

“Sasa kupita wakati mwingine wowote tunahitaji kusimama na Waafghanistan ambao wamebeba gharama ya mizozo, kuwahakikishia kuwa hawajasahaulika”

Shirika la Umoja wa Mataifa la kuhudumia wakimbizi na wakala – UNHCR Pamoja na wakala wa wakimbizi wametoa wito wa jamii za kimataifa kuendeleza mshikamano wa mamilioni ya raia wa Afghanistan ambao wana wasiwasi juu ya maisha yao ya baadae, Pamoja na nchi zilizo wapokea na kuwapa hifadhi baada ya kukimbia machafuko yaliyodumu kwa zaidi ya miongo minne.

Taarifa kwa vyombo vya Habari kutoka Geneva, Uswisi, imesema ombi hilo limetolewa na Indrika Ratwatte, Mkurugenzi wa UNHCR katika ukanda wa Asia na Pasifiki, ambaye amemaliza ziara yake ya wiki moja katika Jamhuri ya Kiislamu ya Iran. 

“ni jukumu la kila mwanajumuiya wa kimataifa kuendelea kushirikiana na Afghanistan katika kuhakikisha amani ya kudumu inapatikana, na kuendelea kusaidia nchi zilizochukua jukumu la kuwapokea wakimbizi wa Afghanistan”. 

Uhaba wa rasilimali na fedha umekuwepo, hata hivyo UNHCR na serikali ya Iran wameendelea kuongoza misaada yao ya kibinadamu. Kwa mwaka huu wa 2021 UNHCR imesema inahitaji jumla ya dola za kimarekani milioni 97.9 lakini mpaka sasa wamepata asilimia 8 tu ya fedha hizo.

Iran imetoa hifadhi kwa mamilioni ya wakimbizi waafghanistan, pamoja na zaidi ya watu milioni 2.6 wasio na nyaraka au pasi za kusafiria za Afghanistan wanaoishi nchini humo. Pamoja na changamoto walizonazo, serikali ya Iran imeonesha mfano mzuri wa utu na mshikamano na wakimbizi.

“Wakimbizi wa Afghanistan wameshuhudia misukosuko mingi katika kipindi cha miongo minne lakini hawajakata tamaa, wana matumaini siku moja wataweza kurudi nyumbani kwao kwa usalama na utu. Kwa miaka kadhaa wamejenga Imani na uthabiti wa kusimama imara wenyewe.” Amesema Ratwatte

Idadi ya watu nchini Afghanistan kwa sasa ni Milioni 35. Mamilioni wakiwa wameyahama makazi yao ndani ya nchi hiyo – watu 100,000 kati yao wakiwa wamehamishwa katika kipindi cha miezi minne mwaka huu pekee. Mamilioni zaidi wakiwa wamevuka mpaka wa nchi hiyo kwa miaka kadhaa, wengi wao wakiishi Iran na Pakistan kama wakimbizi. 

Msaada wa kibinadamu unahitajika kusaidia mamilioni ya wakimbizi wa Afghanistan na jamii zilizowapokea ili kuimarisha hali ya jamii hizi ambazo zimethiriwa kiuchumi na janga la COVID-19

UNHCR imeahidi kuendelea kutoa msaada kwa waafghanista, waliopo ndani na nje ya nchi hiyo.