Poleni sana waathirika tutaendelea kushikamana nanyi:Grandi

21 Agosti 2020

Kamishina mkuu wa shirika la Umoja wa Mataifa la kuhudumia wakimbizi UNHCR, Filippo Grandi amewatembelea wakimbizi ambao ni waathirika wa mlipuko wa wiki iliyopita mjini Beirut nchini Lebanon kuwapa pole na kuwahakikishia kwamba Umoja wa Mataifa utaendelea kushikamana nao kwa hali na mali.

Mjini Beirut mkimbizi kutoka Syria Makhoul Al-Hamad na mwanaye Sama wakichungulia katika moja ya dirisha la nyumba yao lilisambaratishwa kabisa na mlipuko wa Agosti 4 ambapo Sama alijeruhiwa vibaya jicho lake la kushoto na hadi sasa halioni. Makhoul anasema “Kitu kilichoniogopesha sana ilikuwa ni kushuhudia akivuja damu nyingi kwenye jicho baada ya mlipuko, na ilikuwa bayana kwangu kwamba jicho lake limeathirika vibaya.” 

Nyumba yao iko kilometa kama 700 hivi kutoka eneo lilitokea mlipuko na Kamishina mkuu Filippo Grandi ambaye anakamilisha leo ziara yake nchini Lebanon amekwenda kuwatembelea waathirika ambao wakiwemo wahamiaji na wakimbizi na kusikiliza kilio chao.  

Miongoni mwa nyumba alizobisha hodi ni kwa mkimbizi Makhoul Al-Hamad ambaye amesema  “Mlipuko ulipotokea hatukujua endapo bado tuko hai au tunaota. Tulidhani hili linaweza kuwa ni jinamizi tu tunalopitia.” 

Grandi ammepa pole na kutaka kujua endapo Sama amepatiwa matibabu tayari, kisha akapita mitaani kushuhudia hali halisi ya uharibifu katika eneo hilo. 

Kwa mtoto Sama, kwa sasa maisha yake yamebadilika lakini ndoto zake bado ziko palepale  “Napenda shule , ningependa kuwa daktari. Ili keshio kukiwa na mlipuko mwingine kama huu nitakuwa daktari. Na hivyo majeruhi wakija nitawabeba kwenye gari la wagonjwa na kuwaendesha” 

Grandi hii ni ziara yake ya kwanza tangu kufungwa kwa kila kitu kutokana na janga la corona au COVID-19 na amewahakikishia wakimbizi, wahamiaji na waathirika wengine wa mlipuko Lebanon kwamba operesheni za kuwasaidia ndio kipaumbele cha UNHCR, shirika ambalo sasa linatumia dola milioni 35 kuzipa msaada kaya zilizoathirika zaidi na mlipuko huo. 

 

♦ Iwapo ungependa kupokea taarifa kutoka UN News Kiswahili kila wakati zinapochapishwa jisajili  hapa.
♦ Pia unaweza kupakua apu ili kusikiliza matangazo yetu wakati wowote popote ulipo.
♦ Tembelea pia chaneli yetu ya Youtube na pia Soundcloud na Twitter