Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Wahamiaji 9,000 wawasili Hispania katika saa 48, IOM yafuatilia

Waokoaji wa kikosi cha wanamaji cha Italia wakiokoa wahamiaji kwenye bahari ya Mediteranea
Italian Coastguard/Massimo Sestini
Waokoaji wa kikosi cha wanamaji cha Italia wakiokoa wahamiaji kwenye bahari ya Mediteranea

Wahamiaji 9,000 wawasili Hispania katika saa 48, IOM yafuatilia

Wahamiaji na Wakimbizi

Shirika la Umoja wa Mataifa la Uhamiaji, IOM linafuatialiwa kwa wasiwasi mkubwa taarifa za kuwasili kwa wahamiaji wapatao 9,000 huko Ceuta nchini Hispania kati ya tarehe 17 na 19 mwezi huu wa Mei, idadi ambayo shirika hio linasema si ya kawaida katika kipindi hicho kifupi cha siku tatu.

Taarifa ya IOM iliyotolewa hii leo mjini Geneva, Uswisi inasema miongoni kwa wahamiaji hao, 1,500 ni watoto wenye umri wa kati ya miaka 7 hadi 15 na kwamba wengi kati ya watoto hao wameshaunganishwa na familia zao na wengine 800 bado wamepatiwa hifadhi katika bohari huko Ceuta.

Kwa sasa IOM inashawishi mamlaka kujitahidi kuongeza msaada kwa watoto hao huku ikitaka maslahi ya ulinzi wa watoto hao yazingatiwe huku suluhu za kuwasaidia zikiendelea kutafutwa.

IOM imesema iko tayari kusaidia mamlaka za Hispania katika kuwapatia watoto hao misaada inayoendana na mahitaji yao kwa uratibu na wadau walioko mjini Ceuta.

"Hatua zetu za usaidizi zinapaswa kupatia kipaumbele usalama wa wat una hakikisho la kupatiwa ulinzi na aina nyingine za msaada bila kujali kwanza sababu zilizowalazimisha wao kukimbia makwao," amesema Mkurugenzi Mkuu wa IOM António Vitorino.

Amekumbusha kuwa ili usimamizi wa masuala ya uhamiaji na hatua za mahitaji ya wahamiaji yaweze kuwa fanisi, jambo muhimu ni ushirikiano na mashauriano ya dhati kati ya nchi zinazowapatia hifadhi, nchi wanamopita na kule wanakotoka.

Shirika hilo limesema linatambua ushirikiano kati ya Hispania na Morocco na juhudi zao za pamoja za kuimarisha hatua za usimamizi wa masuala ya uhamiaji na hivyo linasihi ushirikiano huo uendelee.

Takriabni watu 26,400 wamewasili nchi za Muungano wa Ulaya au EU kupitia njia ya Mediteranea tangu mwanzo wa mwaka huu wa 2021.

Ingawa idadi imeongezeka ikilinganishwa na kipindi kama hicho mwaka jana, bado IOM inaamini kuwa usimamizi unaweza kuwa bora zaidi kwa kuimarisha kanuni za uhamiaji na usafiri salama na kuboresha mshikamano baina ya nchi za EU.

TAGS: EU, IOM, Wahamiaji na wakimbizi