Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Watu 130 wafa maji Libya baada ya boti kuzama:IOM 

Wafanyakazi wa IOM walihusika na shughuli za uokozi wakati boti lilipozama kwenye ufukwe wa Libya.(Maktaba)
IOM/Hussein Ben Mosa
Wafanyakazi wa IOM walihusika na shughuli za uokozi wakati boti lilipozama kwenye ufukwe wa Libya.(Maktaba)

Watu 130 wafa maji Libya baada ya boti kuzama:IOM 

Wahamiaji na Wakimbizi

Boti iliyozama Pwani ya Libya imeripotiwa kukatili maisha ya watu 130, licha ya kuomba msaada wa dharura wa uokozi limesema shirika la uhamiaji la Umoja wa Mataifa IOM. 

Taarifa ya IOM iliyotolewa leo imesema taarifa za ajali hiyo na vifo imethibitishwa na meli ya kujitolea ya uokoaji ya Ocean Viking, ambayo imepata maiti kadhaa zikielea kaskazini Mashariki mwa mji mkuu wa Libya Tripoli. 

Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa na shirika lisilo la kiserikali, NGO boti iliyozama ilikuwa na matatizo tangu Jumatano asubuhi. 

Msemaji wa IOM, Safa Msehli, amewaambia waandishi wa habari huko Geneva Uswis kwamba waathirika walikuwa walikuwa ndanbi ya boti hiyo kwa siku mbili kabla haijazama katikati mwa  bahari ya Mediterania. 

"Kwa siku mbili, simu ya kengele ya msaada wa dharura ya NGO hiyo , ambayo inahusika kutuma simu za kuomba msaada wa dharura kwa vituo vinavyohusika vya uokoaji wa baharini katika ukanda huo, imekuwa ikitoa wito kwa Mataifa kutekeleza majukumu yao kwa watu hawa na kutuma vyombo vya uokoaji na kwa bahati mbaya, hilo halikutokea. ” 

Zaidi ya watu 500 wamekufa maji kwenye kile kinachoelezwa kuwa ni usafiri kupitia Bahari ya Mediteranea mwaka huu kulingana na takwimu za IOM ikiwa ni karibu mara tatu zaidi ya kipindi kama hicho mwaka jana. 

Wengine wapo katika hatari 

Katika siku tatu zilizopita, kumekuwa na ripoti za boti zingine mbili zilizobeba wahamiaji katikati mwa Mediterania, Bi Msehli alisema. 

Boti moja ilinaswa na mlinzi wa pwani wa Libya na watu 103 au zaidi walirudishwa Libya "na kuwekwa kizuizini", wakati mama mmoja na mtoto walipatikana wakiwa wamekufa ndani ya boti hiyo. 

Boti ya tatu, ambayo inaaminika imebeba watu 40 imekuwa baharini kwa siku tatu na bado haijulikani ilipo, ameongeza msemaji wa IOM. 

"Tunachoogopa ni kwamba mabaya zaidi yametokea, kutokana na hadhi na hali ya boti hizi, ikizingatiwa urefu na muda ambao watu wanatumia katika kile kinachobaki kuwa bahari hatari zaidi ya kuvuka duniani". 

Kulingana na takwimu za IOM, zaidi ya watu 16,700 wamevuka  bahari ya Mediterania tangu kuanza kwa mwaka huu, huku wengine 750 wamekufa maji, ukijumuisha wa ajali ya meli ya Alhamisi. 

TAGS: IOM, ajali ya boti, Mediterranea, Libya, wahamiaji