Wahamiaij wafa maji Mediteranea, siku chache baada ya kupitishwa kwa mkataba wa uhamiaji salama

21 Disemba 2018

Walinzi wa pwani ya Hispania wamapata maiti 12 kutoka kwenye boti zilizonusuriwa kwenye upande wa magharibi wa bahari ya Mediteranea huku watu wengine 33 wakiokolewa kwenye operesheni hiyo ya uokozi iliyofanyika Alhamisi.

Mashirika ya Umoja wa Mataifa yameripoti kuwa watu na maiti hao walipatikana wakati wa operesheni dhidi ya boti 6 ambapo wahamiaji wengine 12 yaripotiwa kupotea baharini.

Halikadhalika wamesema miongoni mwa maiti 12 waliopatikana, 10 ni wanaume na wawili ni wanawake.

Mashirika hayo likiwemo lile la uhamiaji IOM na lile la kuhudumia wakimbizi, UNHCR yanasema bahari hiyo ya Mediteranea ina njia tatu zinazotumiwa na wahamiaji kusafiri ili kufika Ulaya kusaka hifadhi na ukimbizi.

Njia hizo ni ile ya kati iliyopatiwa jina la CMR kutoka Libya kwenda Italia, ile ya mashariki mwa Mediteranea ikimaanisha kuvuka kutoka Uturuki kwenda Ugiriki na ile ya magharibi mwa bahari hiyo inayovuta wahamiaji kutoka Morocco kuelekea Hispania.

Wakimbizi kutoka mataifa ya kusini kwa jangwa la Sahara wakisubiri msaada kutoka kwa chama cha msalaba mwekundu cha Uhispania katika bandari ya Malaga.
© UNHCR/Markel Redondo
Wakimbizi kutoka mataifa ya kusini kwa jangwa la Sahara wakisubiri msaada kutoka kwa chama cha msalaba mwekundu cha Uhispania katika bandari ya Malaga.

 

IOM inasema licha ya kuongezeka kwa idadi ya wahamiaji wanaowasili Ulaya kupitia njia ya magharibi katikati ya mwaka 2017,ni miezi miwili tu iliyopita njia hiyo imeshuhudia ongezeko la wahamiaji wanaopoteza maisha kwa kutumia njia hiyo.

Msemaji wa IOM  huko Geneva, Uswisi Joel Millman, amewaeleza waandishi wa habari hii leo kuwa “tangu majira ya joto kali mwaka 2017 tunashuhudia ongezeko la watumiaji wa njia hiyo kuanzia majira ya joto kali mwaka jana 2017, lakini kinachostaajabisha kuhusu Hispania ni ongezeko la wale wanaopoteza maisha.”

Tukio la jana Alhamisi linakuja siku chache baada ya Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa kuridhia mkataba wa kimataifa wa uhamiaji salama na unaofuata kanuni.

Kwa mujibu wa UNHCR manusura hao hivi sasa wanashikiliwa kwenye kituo kilichoko bandari ya Almeria nchini Hispani na taratibu za usaidizi zinaendelea ikiwemo mchakato wa kuwawezesha kupata hifadhi.

 

 

 

♦ Iwapo ungependa kupokea taarifa kutoka UN News Kiswahili kila wakati zinapochapishwa jisajili  hapa.
♦ Pia unaweza kupakua apu ili kusikiliza matangazo yetu wakati wowote popote ulipo.
♦ Tembelea pia chaneli yetu ya Youtube na pia Soundcloud na Twitter