IOM yapongeza Hispania kwa kukubali kuchukua wahamiaji waliokwama Mediteranea

12 Juni 2018

Hatimaye Hispania imekubali kuchukua zaidi ya wahamiaji 600 waliomo kwenye boti ya Aquarius iliyowaokoa kutoka boti hatarishi baharini Mediteranea.

Wahamiaji hao wakiwemo watoto 120 wasiosindikizwa na wazazi pamoja na wajawazito 7 wamekuwa wakisubiri kwenye chombo hicho tangu jumapili baada ya kila nchi ya Ulaya kukataa kuruhusu meli hiyo kuingia na kutia nanga.

 “Nashukuru kuwa Hispania imeingilia kati na kupata suluhu ya janga hili, lakini nina hofu kubwa kuwa sasa nchi zinaanza kukataa wahamiaji waliookolewa,” amesema Mkurugenzi Mkuu wa shirika la uhamiaji la Umoja wa Mataifa, William Swing.

Amesema kuwaweka baharini wahamiaji waliookolewa hakutakatisha tamaa wahamiaji wanaosaka hifadhi Ulaya.

Hispania ilichukua uamuzi huu baada ya kuonekana kuwa hali ya hewa inazidi kuwa mbaya na hofu inaongezeka kuhusu ustawi wa wahamiaji hao walio katika mazingira duni.

Hata hivyo boti hiyo itahitaji kati ya siku tatu au nne kufikia bandarini na kutia nanga.

IOM inaamini kuwa nchi za Muungano wa Ulaya, EU zinapaswa kuchukua hatua zaidi kusaidia mataifa yaliyo karibu na bahari ya Mediteranea katika suala la uhamiaji.

Bwana Swing amesema kuokoa maisha ya watu kunapaswa kuwa jambo linalopatiwa kipaumbele na kwamba ni lazima kusaka mbinu kusaidia wahamiaji waliookolewa na kufanya kazi zaidi kusaidia wahamiaji walioko Ulaya.

Na kwa mantiki hiyo IOM imesihi EU iangalie upya mapitio ya kanuni ya Dublin ili kuhakikisha nchi hizo zina mshikamano na kuheshimu vipengele kuhusu mikataba ya kimataifa ya uhamiaji.

 

Shiriki kwenye Dodoso UN News 2021:  Bofya hapa Utatumia dakika 4 tu kukamilisha dodoso hili.

♦ Na iwapo ungependa kupokea taarifa kutoka UN News Kiswahili kila wakati zinapochapishwa jisajili  hapa.
♦ Pia unaweza kupakua apu ili kusikiliza matangazo yetu wakati wowote popote ulipo.
♦ Tembelea pia chaneli yetu ya Youtube na pia Soundcloud na Twitter