Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Muungano wa Ulaya na Libya zatakiwa kurekebisha sera za uokoaji Mediteranea

Wahamiaji wakiokolewa baada ya kuvuka bahari ya Mediteranea.
PICHA: IOM/Francesco Malavolta (maktaba)
Wahamiaji wakiokolewa baada ya kuvuka bahari ya Mediteranea.

Muungano wa Ulaya na Libya zatakiwa kurekebisha sera za uokoaji Mediteranea

Wahamiaji na Wakimbizi

Kamishna Mkuu wa Haki za Binadamu kwenye Umoja wa Mataifa Michelle Bachelet ametoa wito kwa serikali ya Umoja wa Kitaifa nchini Libya na Muungano wa Ulaya, EU  Pamoja na nchi wanachama wa Umoja huo kurekebisha haraka mfumo, sera na kanuni za sasa za  kusaka na kuokoa watu kwenye bahari ya Mediteranea kwa kuwa mifumo ya sasa inapora haki za uhai na utu za wahamiaji.

“Kila mwaka watu wanazama na kufa maji kwa sababu msaada wa kuwaokoa unachelewa kufika, au wakati mwingine, haufiki kabisa,” amesema Bi. Bachelet kupitia taarifa iliyotolewa leo na ofisi yake mjini Geneva, Uswisi, ikinukuu ripoti ya Ofisi ya Haki za Binadamu ya Umoja wa Mataifa kuhusu Usakaji na Uokoaji na ulinzi wa wahamiaji katika eneo la Mediteranea ya Kati.

Kamishna huyo amesema hata wale wanaookolewa wakati mwingine husubiri kwa siku kadhaa au wiki kuweza kuteremka salama kutoka kwenye chombo kilichowaokoa au wanajikuta wanarejeshwa Libya, nchi ambayo si salama kwa sasa.

Kwa mujibu wa Kamishna huyo, vifo vingi vya wahamiaji vinavyotokea  katika bahari ya Mediteranea vinaweza kuepukwa.

Ripoti hiyo inanukuu ushahidi ukidokeza kuwa ukosefu wa ulinzi wa haki za binadamu za wahamiaji baharii si janga  lisilo la kawaida, bali ni matokeo ya maamuzi na sera za kina za mamlaka za Libya, Muungano wa Ulaya, EU nchi wanachama wa Muungano huo, taasisi na wadau wengine ambapo wameweka mazingira ambamo kwayo utu na haki za binadamu za wahamiaji ziko hatarini.

Ripoti hiyo, ambayo inajumuisha kipindi cha kuanzia mwezi Januari mwaka 2019 hadi Desemba mwaka 2020 imeonesha wasiwasi kwa kuwa EU na wanachama wake wamepunguza kwa kiasi kikubwa operesheni zao za kusaka na kuokoa wahamiaji wanaotumia bahari ya Mediteranea kuvuka kwenda kusaka Maisha bora Ulaya, huku mashirika ya kiraia ya kibinadamu  yakizuiwa kufanya operesheni za uokozi.

Na kama hiyo haitoshi, meli za kibiashara kwa kiasi kikubwa zinaepuka kusaidia wahamiaji walio hatarini kwa sababu ya kucheleweshwa au mvutano kati yao na mamlaka wakati wanapofika bandari salama ili kushusha wahamiaji hao waliowaokoa.

Kuchelewa huko kumekuwa na hali mbaya zaidi mwaka 2020 wakati wa janga la Corona au COVID-19 ambapo wahamiaji walilazimishwa kusalia kwenye karantini baharini na hata waliposhuka walikumbwa na kuswekwa korokoroni kwa muda.

Bi Bachelet amesema hali ya watu kusafiri kinyume cha sheria itaendelea hadi pale ambapo kutakuwepo na njia na kanuni salama za uhamiaji hivyo ameiomba EU kuonesha mshikamano na kuhakikisha nchi zilizo karibu na bahari ya Mediteranea kama vile Malta na Italia haziachwi peke yao kubeba mzigo wa uwajibikaji kwa wahamiaji.