Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu
Mwanamke na watoto wake wakiwa wamesismama kwenye mlango wa makazi yao ya muda kwenye mji wa Ibb Yemen :Kutoka maktaba

Takriban Wakimbizi 300,000 wapata maambukizi ya virusi vya Corona mwaka 2020

IOM/Olivia Headon
Mwanamke na watoto wake wakiwa wamesismama kwenye mlango wa makazi yao ya muda kwenye mji wa Ibb Yemen :Kutoka maktaba

Takriban Wakimbizi 300,000 wapata maambukizi ya virusi vya Corona mwaka 2020

Wahamiaji na Wakimbizi

Takriban wakimbizi 300,000 kutoka Mashariki na Pembe ya Afrika, wamepata maambukizi ya virusi vya Corona au COVID-19 kwa mwaka 2020. Idadi hiyo imetajwa kwenye ripoti kuu ya mwaka 2020 ya Shirika la Umoja wa Mataifa la Uhamiaji, IOM, kwa bara la Afrika iliyotolewa wiki hii.

Taarifa ya IOM kutoka Nairobi Kenya, imeangazia matokeo mabaya ya janga la Corona kwa wahamiaji walio kwenye mazingira magumu, wahamiaji wa ndani, wakimbizi wanaotafuta hifadhi, watoto walio peke yao, wakimbizi wanaorudi na wale waliokwama.

Mohammed Abdiker, Mkurugenzi wa IOM, Kanda ya Mashariki na Pembe ya Afrika amesema, "Tunaposonga mbele tunatakiwa kuimarisha njia za uhamiaji wa kawaida na kuhamasisha uendelezaji wa wahamiaji wanaorejea nyumbani".

Maelfu ya wakimbizi, wengi wao kutokea Ethiopia wamekwama huko Djibouti, Somalia na Yemen, wakishindwa kuendelea na safari yao ya kwenda Saudi Arabia kupitia Yemen. Kwa mujibu wa taarifa, idadi ya watu wanaovuka Yemen kutokea Pembe ya Afrika imepungua kwa kiwango kikubwa, kutoka watu 138,000 hadi watu 37,000 sawa na upungufu wa zaidi ya asilimia 73 ikilinganishwa na mwaka 2019.

Abdiker amesema ili suluhu ipatikane ni lazima udhibiti wa wahamiaji kuimarishwa, "Tunahitaji kuona juhudi za kudhibiti uhalifu wa kikanda na kimataifa ambao utahusisha usafirishaji wa wakimbizi na utoroshaji wa watu katika Kanda. Bila ya hivi juhudi zinazofanywa na nchi wanachama kudhibiti uhamiaji zitaendelea kudhoofishwa na wahamiaji wataendelea kuteseka"

Mamia ya maelfu ya watu katika ukanda wa mashariki na Pembe ya Afrika wanaupungufu wa chakula, maji, ulinzi na dawa. Pia vifaa vya kujilinda dhidi ya maambukizi ya COVID19 ni vichache na kwasasa hawana namna ya kufikiwa na chanjo ya Corona.

Ripoti hiyo imehitimisha kwa kusema wakati chanzo cha wakimbizi kwa Upande wa Mashariki na Pembe ya Afrika ni umasikini, machafuko na matukio yanayosababishwa na athari za mazingira, janga la Corona limeongeza tabu Zaidi kutokana na uchumi kuathirika vibaya.

Hoja ya ripoti hiyo ya IOM inaungwa mkono na ripoti ya hivi karibuni ya Shirika la Maendeleo la Umoja wa Mataifa ambayo limeeleza athari za muda mrefu za kiuchumi na kijamii zilizosababishwa na COVID-19 zitaongeza wigo wa umaskini baina ya nchi na athari Zaidi zinaelezwa zitatokea kwa watu waishio barani Afrika.