Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

IOM/UNHCR watangaza kusitisha safari za wakimbizi sababu ya COVID-19

Theluthi mbili ya wakimbizi wa ndani kwenye kambi ya Kobiteye nchini Chad ni watoto
© OCHA/F. Gabellini
Theluthi mbili ya wakimbizi wa ndani kwenye kambi ya Kobiteye nchini Chad ni watoto

IOM/UNHCR watangaza kusitisha safari za wakimbizi sababu ya COVID-19

Afya

Wakati nchi zikibana idadi ya watu wnaoingia nchini mwao kwa sababu ya janga la kimataifa la virusi vya Corona , COVID-19 na kuweka vikwazo dhidi ya safari za kimataifa za anga , mpango wa kuwasafirisha wakimbizi kwenda kwenye makazi mapya sasa umeingia dosari.

Hayo ni kwa mujibu wa taarifa ya pamoja ya shirika la Umoja wa Mataifa la kuhudumia wakimbizi UNHCR na lile la wahamiaji IOM, ambayo imeongeza kwamba baadhi ya nchi zimesitisha mpango wa kuwapokea wakimbizi kwa ajili ya kuwapa makazi kutokana na hali ya afya ya umma ambayo inaathiri uwezo wao wa kupokea wakimbizi wapya.
Mamia ya familia za wakimbizi zimeathrika na hali hii na sharia zinazobadilika haraka kuhusu safari zao huku wengine wakikabiliwa na kusubiri muda mrefu na wengine wakikwama  au kutenganishwa na watu wa familia zao.
Mashirika hayo ya UNHCR na IOM, yamesema yanatiwa hofu kwamba safari za kimataifa zinaweza kuwaweka wakimbizi katika hatari zaidi ya kupata virusi vya Corona.
Na hivyo mashirika hayo yanachukua hatua za kusitisha safari za kwenda kuwapa makazi mapya wakimbizi. Hizi ni hatua za muda ambazo zitaendelea tu pale ambapo ni muhimu na inapohitajika.

Wakati mpango wa kuwapa makazi ya kudumu wakimbizi ukisalia kuwa ni nyenzo muhimu kwa wakimbizi wengi UNHCR na IOM wanatoa wito kwa nchi  na kushirikiana nazo kwa karibu ili kuhakikisha kwamba safari hizo zinaendelea kwa kesi ambazo ni za dharura kadri iwezekanavyo.
Hatua hiyo itaanza kutekelezwa siku chache zijazo wakati mashirika hayo yakijaribu kuwasafirisha wakimbizi ambao safari zao zimeshakamilika kwenda walikopangiwa.
Mpango wa makazi ya kudumu kwa wakimbizi unaokoa Maisha hasa kwa wakimbizi wasiojiweza na IOM na UNHCR wataendelea kufanyakazi na nchi zinazowahifadhi  na wadau wengine muhimu kuhakikisha kwamba mchakato wa kesi hizo unaendelea.
“Pia tutaendelea kuwasiliana na wakimbizi na mashirika yote yanayofanyakazi kusaidia wakimbizi ili kuendelea kusaidia mpango huu muhimu.”
Mashirika yote yanatarajia kuanza tena mchakato huo mapema hali itakaporuhusu.