Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Wataalam wa UN waishutumu Tanzania na Burundi

Wakimbizi wa Burundi wanaorejea nchini mwao kutoka Tanzania wakiwa kwenye kituo cha mpito cha Mabanda katika jimbo la Makamba nchini Burundi. (24 Aprili 2018)
OCHA/Christian Cricboom
Wakimbizi wa Burundi wanaorejea nchini mwao kutoka Tanzania wakiwa kwenye kituo cha mpito cha Mabanda katika jimbo la Makamba nchini Burundi. (24 Aprili 2018)

Wataalam wa UN waishutumu Tanzania na Burundi

Haki za binadamu

Wataalam wa haki za binadamu wa Umoja wa Mataifa leo Aprili 13, 2021, mjini Geneva Uswisi wamezitaka serikali za Tanzania na Burundi kuheshimu haki za wakimbizi na waomba hifadhi ambao wamekimbia Burundi. 

Wataalamu hao wamelalamikia madai ya uwepo wa ripoti za kutoweka kwa watu, kuteswa, kurudishwa kwa nguvu na ukandamizaji. 

Kukamatwa kiholela na kutoweka kunadaiwa kutekelezwa na polisi wa Kitanzania na ushirikiano wa  kijasusi wa pande zote mbili yaani Tanzania  na Burundi, wataalam wa Umoja wa Mataifa wamesema.  

"Mbali na sera kali za kambini zilizowekwa na Serikali ya Tanzania, wakimbizi wa Burundi na waomba hifadhi sasa wanaishi kwa hofu ya kutekwa nyara usiku na vikosi vya usalama vya Tanzania na kupelekwa kusikojulikana au kurudishwa kwa nguvu kwenda Burundi.” Wataalam wamesema. 

Wapinzani wa kisiasa wa Burundi wamedaiwa kufuatiliwa miongoni mwa wakimbizi na watu wanaotafuta hifadhi nchini Tanzania. Hali ya usalama katika kambi hizo inaonekana kuathirika sana huku kukiwa na ripoti kwamba mawakala wa ujasusi wa Burundi wanaojifanya wakimbizi ndani ya kambi hizo wanatambua watu maalum ambao baadaye wanakamatwa na vikosi vya usalama vya Tanzania. 

Wataalamu hao wametoa wito wakise, "serikali ya Burundi inapaswa kuacha ukandamizaji wake dhidi ya raia wake ikiwa ni pamoja na wale wanaotafuta ulinzi wa kimataifa nchini Tanzania."  

Wakimbizi wamethibitisha kuchukuliwa na polisi wa Tanzania, kutoweshwa, kuteswa kabla ya kushurutishwa kusaini 'kurejea kwa hiari' nchini Burundi. Wengine wamehojiwa kuhusu madai ya kuwa wana uhusiano na makundi yenye silaha au kwama wao wanamiliki silaha. Pia wamehojiwa kuhusu shughuli zao kwenye kambi na wakati mwingine wakitakiwa kutoa pesa ili waachiwe.  

"Tumesitushwa sana na ripoti kwamba wakimbizi wengine wa Burundi wameuawa baada ya kutekwa nyara na vikosi vya usalama vya Tanzania." Wataalam hao wameongeza.  

Vilevile wataalamu hao wameeleza kuwa kuongezeka kwa wasiwasi juu ya usalama kumesababisha wengi kurudi Burundi kwa hofu badala ya nia ya kweli ya kurudi nchi yao ya asili. 

"Inakatisha tamaa sana kwamba tangu Serikali itangaze mnamo Agosti 2020 kwamba uchunguzi juu ya upotezaji huo hakuna matokeo yoyote ambayo yamewekwa wazi kwa umma. Serikali ya Tanzania inajua hali hiyo na lazima ichukue hatua zote muhimu kukomesha mara moja na kurekebisha ukiukaji huo." Wamehitimisha wataalamu hao wa Umoja wa Mataifa wanaoangazia masuala yanayokiuka haki za binadamu kama vile utoweshwaji, mateso, kulazimishwa kuhama na ukamatwaji holela usio wa haki.